Wafanyabiashara waiomba serikali kuwasaidia mitaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:06 PM Oct 14 2024
Katibu Mtendaji wa NEEC, Being’i Issa
Picha: Mtandao
Katibu Mtendaji wa NEEC, Being’i Issa

BAADHI ya wafanyabiashara mkoani Kagera wameiomba serikali kusaidia kundi la wanawake,vijana na wenye ulemavu kukuza mitaji itakayosaidia waweze kujiendeleza katika uzalishaji na upanuzi wa biashara zao.

Uwezeshwaji wa mitaji utasaidia kukidhi mahitaji, na kuachana fikra za kutumia akiba ambazo tayari wameshatunza kama sehemu ya faida kwa kile ambacho kimepatikana.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hii jana, walisema hali hiyo imesababisha kutokukua kwa biashara au ujasiriamali na kufanya warudi nyuma ikiwa tayari amefika hatua ya kutambuliwa na wateja.

Wamezungumza jana Oktoba 12,2024 wakati wa uzinduzi wa programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (IMASA), kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshwaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) iliyowakutanisha wafanyabiashara mbalimbali mkoani Kagera.

Adivela Raulent mjasiriamali wa zao la dagaa Kisiwani Goziba amesema matamanio yanakina mama ni kuwa na mitaji ili wapanue biashara kwa kupata mtaji zaidi.

"Nimebuni biashara nimefanya nimeona inasoko kinachonikwamisha ni mtaji utakaonisaidia zaidi kufikia wateja wengi zaidi,bidhaa inapatikana lakini tatizo ni vifaa vya kuboresha na kufanya muda wote bidhaa inakuwepo,"amesema Raulent.

Aidha, amesema mjasiriamali anaingia katika mikopo ya  kila wiki na nyakati nyingine zinakuwa ngumu katika biashara anashindwa kuhimili mikopo huo, kufanya kwenda tofauti na malengo.

Prospa Clement mfanyabiashara wa nafaka soko la Bukoba amesema tatizo la mitaji na maarifa ya biashara yanawakumba wengi kwa kuwa wanaingia kwenye ujasiriamali hawana uelewa na jambo analo lifanya.

Aidha, amesema ni vyema sasa mikopo inapotolewa iwe sambamba na elimu kusaidia anayekwenda kuboresha shughuli yake afanye nini ili kukua kiuchumu.

Katibu Mtendaji wa NEEC, Being’i Issa amesema moja ya majukumu ya progaramu ni kufanyia kazi kwa pamoja na kufanya vipimo vya mafanikio ya wananchi kwani wengi hawafamu fursa zinapatikana serikalini.

Amesema lengo kuu ni kufanya uwezeshaji wa uchumi kwa wananchi hasa wale ambao tayari wameshakuwa na shughuli za kufanya katika uchumi.

Amesema uwezeshwaji huo utaenda sambamba na utoaji wa mikopo na kijenga uwezo, kwani programu inafanya shughuli za uongozi wa mikoa na halmshauri 

"Ujengaji wa maarifa na upatikanaji wa fursa ni mambo ambayo yatafanyiwa kazi na serikali nani sehemu ya msingi yenye kumfahamisha mwananchi kujua zaidi,"amesema Issa.

Vilevile amesema kupitia uongozi wa wilaya na mkoa programu itaangalia ni mambo gani wananchi wanahitaji kusaidiwa, ili kuona kwamba mikopo inayotakiwa na inayotolewa isaidie eneo husika.