Mbunge ataka muswada kufumua Sheria ya Ndoa upelekwe bungeni

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 11:06 AM Oct 14 2024
MBUNGE wa Singida Mjini, Mussa Sima
Picha:Mtandao
MBUNGE wa Singida Mjini, Mussa Sima

MBUNGE wa Singida Mjini, Mussa Sima ameomba Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Wenye Mahitaji Maalum, kupeleka bungeni muswada wa kurekebisha Sheria ya Ndoa, ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni.

Sima ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yaliyoandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) na kushirikisha wasichana na wadau kutoka mikoa mbalimbali nchini. 

Sima alisema kuwa huu ndio wakati mahususi kwa wizara hizo za kisekta zinazohusika katika eneo hilo, kufanyia kazi sheria hiyo. 

"Kazi kubwa ya wabunge ni kushauri serikali, nitoe wito sasa kwa mawaziri wa kisekta, huu ndio wakati wa kutuletea muswada, tuchakate, upelekwe bungeni na wabunge wapate nafasi ya kuchangia, kupata mawazo mbadala ili jambo hili litekelezeke. 

"Sasa hivi kuna utata sana kuhusu umri sahihi wa mtoto wa kike kuolewa, tunaona mtandao wa elimu Tanzania na wadau wengine wameamua kwa dhati kuleta chachu ya mabadiliko ya kutaka mtoto wa kike atimize ndoto yake, wakihamasisha juu ya ulinzi wake dhidi ya ukatili na unyanyasaji," alisema. 

Kuhusu baadhi ya wazazi kuwatumia watoto wao wa kike kama kitega uchumi, Sima aliwataka wabadili mitizamo yao na kuwawezesha watimize ndoto zao za kufika mbali kielimu. 

Mratibu wa TEN/MET, Martha Makala, alisema wanaendelea kuelimisha jamii kuhakikisha watoto wanakwenda shuleni na kupata haki yao ya elimu. 

"Wazazi, walezi na jamii pia tuhakikishe watoto wanapata chakula shuleni. Kama sisi tunavyokula majumbani, ndivyo hivyo tuwathamini watoto wetu, ili wasikae na njaa na itawashawishi wapende kubaki shuleni na wasiingie kwenye vishawishi vingine kwa sababu ya njaa," alisema Martha.