Samia kuzindua kitabu cha historia ya Mwenge

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 12:21 PM Oct 14 2024
Mwenge wa Uhuru.
Picha: Mtandao
Mwenge wa Uhuru.

RAIS Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuongoza Watanzania nchini katika maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru yatakayotanguliwa na kumbukizi ya miaka 25 ya kifo cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere pamoja na uzinduzi wa Kitabu cha Historia ya Mwenge huo.

Akizungumza leo Oktoba 13,2024 mara baada ya kukagua maandalizi ya maadhimisho hayo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema maandalizi yamekamilika na ameridhishwa nayo.

“Baada ya kukagua nimeridhishwa na maandalizi ya maadhimisho haya ambayo mgeni wetu rasmi atakuwa Rais Samia Suluhu Hassan na ataongoza watanzani katika shughuli mbalimbali zizotarajiwa kufanyika hapa kesho (leo),”amesema Majaliwa.

Aidha, amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwan Kikwete kwa kushirikiana na kamati ya maandalizi kuhakikisha wanamalizia taratibu zote zilizosalia katika maandalizi hayo mapema iwezekanavyo.

Awali, akitoa taarifa ya maandalizi ya maadhimisho hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwan Kikwete amesema yataambatana mambo mbalimbali katika maadhimisho hayo.

Ridhiwani ametaja mambo hayo yatakayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ni pamoja na ibada ya kumbukizi ya kifo cha Hayati Mwalimu J.K.Nyerere ambayo itafanyika katika Kanisa Katoliki la Parokia ya Mt.Fransisco wa Exavery  Nyakahoja jijini Mwanza kuanzia saa moja kamili Asubuhi.

Kadhalika, amesema atatembelea na kukagua maonesho ya wiki ya Vijana yanayoendelea katika Viwanja vya Furahisha, kuongoza shughuli za kilele cha mbio za Mwenge na kuzindua Kitabu cha Falsafa ya Mwenge wa Uhuru kilichoandikwa na miongoni mwa Mawaziri wa Baraza la Mawaziri, Job Lusinde na kuhaririwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM na Mbunge wa Kuteuliwa, Dk. Bashiru Ally.

Aidha, ametaja mambo yatakayofanyika katika maadhimisho ya kilele cha mbio za mwenge ni pamoja na maonesho ya alaiki ya watoto mkoani Mwanza,  burudani ya nyimbo na muziki, utenzi na utamaduni, kuhutubia watanzania.

“Vilevile Rais atatoa vyeti vya zawadi, tunu mbalimbali za mashindano ya mbio za mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2024 pia atahitimisha mbio hizo kwa kupokea taarifa ya kiongozi wa mbio hizo Taifa na kuwapatia vyeti wakimbiza mwenge,”amesema Ridhiwani.

Ridhiwani amesema mwisho Rais Samia atahitimisha kwa kukabidhi Mkuu wa Majeshi (CDF) Bendera ya Taifa pamoja na mwenge wa uhuru kwa hatua ya kuvipeleka katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro.