Majaliwa atoa maelekezo mahususi kukabili ukame

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 02:17 PM Oct 14 2024
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Picha:Mtandao
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imetoa maelekezo mahususi kwa mamlaka zake kupitia kamati za usimamizi wa maafa kuhakikisha kuna udhibiti wa matatizo yanayoweza kujitokeza kutokana na mvua chache za vuli.

Aidha, amesema taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), zinaonyesha kuwa Tanzania itaendelea kukosa mvua za vuli zilizotarajiwa kuanza mwezi huu hadi Desemba, hali itakayosababisha taifa kukosa mavuno ya kutosha.

Aidha, alisema serikali imeweka mikakati kuhakikisha kunakuwa na udhibiti wa hali hiyo pasitokee madhara makubwa kwa wananchi.

Majaliwa alitoa kauli hiyo jana Oktoba 13,2024  jijini Mwanza katika maadhimisho ya Wiki ya Siku ya Maafa Duniani.

 “Welekeo huu unaonesha kwamba maeneo mengi ya nchi yanayopata mvua hizo yatakosa mvua za kutosha na katika kukabiliana na kurejesha hali hiyo maeneo yote yanatakiwa kuchukua tahadhari na wananchi wote wachukue tahadhari,” alisema Majaliwa.

Aidha, alitoa maelekezo sita kwa mamlaka husika kuhakikisha wanafanya jitihada za urejeshwaji wa hali ya kawaida ikiwa ni pamoja na mamlaka husika kuendelea kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi pamoja na utunzaji wa chakula cha binadamu na malisho ya mifugo.

Pia aliagiza kuimarishwa utoaji wa taaluma ya mbinu za kilimo zinazohitajika hasa kwa kutumia maji kidogo, tatu taasisi za umma zikiwemo za elimu, afya ofisi za mikoa pamoja na wilaya na sekta binafsi kupanua na kuweka mifumo ya kuna na kuhifadhi maji ya mvua.