Zahanati iliyotumia tochi ya mlinzi kuhudumia wagonjwa yapata umeme

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 11:21 AM Oct 14 2024
Zahanati iliyotumia tochi ya mlinzi kuhudumia wagonjwa yapata umeme
Picha: Shaban Njia
Zahanati iliyotumia tochi ya mlinzi kuhudumia wagonjwa yapata umeme

SIKU sita baada ya kuripotiwa na gazeti hili Zahanati ya Rwakaremera kutokuwa na umeme, hatimaye serikali imepeleka huduma hiyo katika zahanati hiyo.

Septemba 5, mwaka huu, Nipashe iliripoti kuwa zahanati hiyo ya kijiji cha Rwakaremera, kata ya Kasulo, wilaya ya Ngara, mkoani Kagera haikuwa na umeme, hivyo nyakati za usiku watoa huduma wake kulazimika kuhudumia wagonjwa wakitumia tochi ya mlinzi wa zahanati.

Ni zahanati iliyoasisiwa na wakazi wa kijiji hicho waliochangishana Sh. 20,000 kwa kila kaya na kupata jumla ya Sh. milioni 30 na kuanza ujenzi wake mwaka 2021, kwa kujenga boma na baadaye serikali ikatoa Sh. milioni 50 za ukamilishaji wake na mwaka uliofuata ikaanza kutoa huduma.

Yusufu Katura, Diwani wa Kasulo anasema kuwa Septemba 11, mwaka huu, ikiwa ni siku sita baada ya Nipashe kuripoti kuhusu hali hiyo inayokinzana na miongozo ya kitaifa ikiwamo Sera ya Afya (2007), serikali ilipeleka huduma ya umeme katika zahanati hiyo.

Anasema upatikanaji nishati hiyo katika zahanati hiyo umesaidia kuondoa malalamiko ya wananchi ya kukosa huduma nyakati za usiku, wanapokuwa na wagonjwa wa dharura, wakiwamo wajawazito.

Diwani Katura anasema kuwa kila kikao cha Baraza la Madiwani, alikuwa anawasilisha hoja kuhusu suala la zahanati hiyo kutokuwa na umeme na kupewa ahadi zisizotekelezwa kwamba ingeunganishiwa huduma hiyo.

"Gazeti Nipashe lilipoandika kwamba zahanati yetu haina nishati ya umeme, suala hili lilifanyiwa kazi haraka na sasa hakuna tena malalamiko ya wananchi.

"Septemba 5, mwaka huu, Nipashe ilitoa taarifa juu ya namna wagonjwa wanavyopata adha kwa kuhudumiwa kwa kutumia tochi ya mlinzi wa zahanati. Siku iliyofuata (Septemba 6, 2024) mashimo ya nguzo yalianza kuchimbwa na kuwekwa nguzo na tarehe 11 Septemba umeme uliwaka kwa mara ya kwanza kituoni na huduma zinaendelea kutolewa," Diwani Katura anapongeza hatua zilizochukuliwa.

Anabainisha kuwa zahanati hiyo inahudumia vitongoji vya Kamula na Ngoma, kijijini Rwakaremera.

Mwonekano wa ndani wa Zahanati ya Rwakaremera baada ya kupata nishati ya umeme. PICHA ZOTE: SHABAN NJIA.

"Sasa huduma za afya zimeboreshwa na wagonjwa wanapata matibabu mchana na usiku. Changamoto iliyopo hivi sasa katika zahanati hiyo ni uhaba wa mabenchi.

"Tutakaa kikao cha Kamati ya Maendeleo ya Kata ili kuangalia namna ya kutatua changamoto ya uhaba wa mabenchi kwa ajili ya kukaa wagonjwa, kilio chao kikubwa kimeshatatuliwa," anasema.

Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Dk. John Samweli, anasema kupatikana nishati ya umeme kituoni, kumesaidia kuwaondolea adha ya kutumia tochi ya mlinzi na simu janja zao nyakati za usiku, akiitaja ilikuwa kero kuu kwa wananchi, hasa wajawazito na watoto waliohitaji huduma za dharura kituoni usiku.

"Umeme kwa mara ya kwanza umewaka kwenye zahanati hiyo Septemba 11, mwaka huu na wananchi walikuwa wakishuhudia na walifurahi sana, walisikika wasema 'hatutahudumiwa kwa tochi ya mlinzi tena'. Sisi wenyewe umeme umeturahisishia utoaji huduma," anasema.

Dk. Samweli anafafanua kuwa hivi sasa zahanati hiyo ina watoa huduma wanne ambao ni mtaalamu wa maabara, muuguzi, ofisa afya msaidizi na Mganga Mfawidhi.

"Hatutaki tena kusikia wananchi waliojitoa na kujenga zahanati hii wakilalamika kwa kukosa huduma nyakati za usiku," anasema. 

Mganga Mfawidhi huyo anasema changamoto iliyopo ni ukosefu wa mabenchi kwa ajili ya wagonjwa. Hivi sasa wanayo sita; mawili yanatumika na wagonjwa wa nje (OPD) na manne yanatumiwa na wajawazito wanaohudhuria kliniki na kuna wakati wagonjwa wanalazimika kuketi chini ya miti inayozunguka zahanati.

Anasema wanatarajia kutenga sehemu ya mapato ya zahanati, ili kuongeza mabenchi matano kwa ajili ya wajawazito na wagonjwa wa nje.

1

Anasema wagonjwa kwa sasa ni wengi, wakiwa na wastani wa kuhudumia wajawazito 30 hadi 50 kwa mwezi, japo kuna miezi wanahudumia hadi wajawazito 80 kwa mwezi.

Shadia Abdully, mkazi wa kitongoji cha Njiapanda, anapongeza serikali kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu na kupeleka nishati ya umeme kwenye zahanati waliyojenga kwa kuchangishana fedha.

Anasema waliokuwa wakipata adha hiyo ni wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano , kwa kuwa ndiyo kundi linalohitaji zaidi huduma za dharura usiku.

Mkazi wa kitongoji cha Ngoma, Ramadhani Ruzuba anasema kuwa mwaka jana, mkewe alijifungulia njiani na kuzalishwa na watu wasiokuwa na taaluma ya uuguzi wakati wakienda zahanati ya kijiji jirani kutokana na zanahati yao kukosa umeme.

"Sasa hatutarajii kupata adha hii tena kwa kuwa umeme umepatikana na watoa huduma watakuwa wanahudumia hata nyakati za usiku," anasema.

John Nkwale, mlinzi wa zahanati hiyo anasema kuwa tangu zahanati ipate umeme, ameshuhudia wajawazito sita wa dharura wakipatiwa huduma usiku na muuguzi.

"Wote wamepatiwa huduma bila manung'uniko tofauti kabisa na ilivyokuwa awali. Zamani walipohudumiwa kwa tochi yangu na simu janja zao wauguzi, walinung'unika mno," anasimulia.

Sera ya Afya ya Mwaka 2007 na Mpango wa Maendeleo wa Afya ya Msingi (2008), vinaelekeza serikali kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati, kila kata iwe na kituo cha afya, kila wilaya iwe na hospitali ya wilaya na mkoa uwe na hospitali ya rufani ya mkoa. Pia vituo hivyo vya kutolea huduma viwe na miundombinu inayokidhi matakwa ya utoaji huduma za afya.

2