MIAKA 25 BILA YA NYERERE : Malecela: Sitosahau ile siku alinituma kumuona Amin, niliona maisha rehani

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 11:35 AM Oct 14 2024
Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela na  Idi Amin.
Picha:Nipashe Gazeti
Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela na Idi Amin.

NI majira ya saa 10 jioni ya Alhamis wiki iliyopita, nipo nyumbani kwake Mtaa wa Kilimani jijini Dodoma, mbele yangu yupo Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela mwenye umri wa miaka 90.

Mguuni ana viatu vya vijana ‘raba’, shati la kitenge, akiwa ametoka shambani kwake Chinangali, wilayani Chamwino wastani wa kilometa 30.  

Anatukaribisha kwa kauli: “Samahani sana nimechelewa kurudi kutoka shambani, ili tufanye mahojiano, kama ambavyo mliomba. Ilikuwa muhimu kwenda kule shambani. 

“Nilikwenda asubuhi, ili niwahi kurudi, maana katika shamba letu la ushirika leo tulikuwa tunakutana na Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ushirika. Karibuni sana ofisini kwangu,” Mzee Malecela anatamka kwa bashasha la ukarimu. 

Baada ya hapo anaketi, kisha anaamka kijasiri anatoka nje akisema: “Kabla ya kuanza mazungumzo yetu, ngoja nifuatilie kwanza soda, ili mlainishe makoo yenu. (alimuita Msaidizi wake) nileteeni soda na maji kwa ajili ya wageni wangu au ‘can you have a glass of wine? (mnaweza kupata kinywaji mvinyo?)” 

Alipojibiwa kuwa soda inatosha, anarejesha masihara yaliyobeba maana kwa mwanahabari mpiga picha (Peter Mkwavila): “Umemuona Yesu? Lakini nitakupa kitabu kimoja utakisoma siku nyingine....

 “Kimeandikwa na Myahudi anasema hivi nyie dunia nzima mna ugonjwa gani? ....Huyu mwandishi ameandika historia fupi ya ‘humankind’ wanadamu walitoka wapi? Anasema wataalamu wote duniani wanakubaliana kwamba mtu wa kwanza alitoka Olduvai Gorge...”  

Hapo ndipo anaanza simulizi yake, alivyomfahamu Nyerere kwa karibu, akisema mambo makuu kadhaa. 

Mosi, anasema alikuwa mnyenyekevu, mwenye huruma, upendo, unyenyekevu na mtiifu., akiendelea: “Mwalimu Nyerere wakati mwingine alikuwa anaweza kuvaa shati bila vesti.  

“Alikuwa mnyenyekevu, mtiifu, anayependa watu. Nikupe mfano mmoja tulikwenda Canada sasa tukiwa pale jioni kulikuwa na TV (runinga), kwa hiyo mimi nikaenda nikaifungua. 

“Baada ya kufungua kulikuwa na ngumi wakati huo, alikuwa anampiga mwenzake sana, Mwalimu akasema ‘John, John zima! hiyo kwanini mnaangalia vitu vya kikatili namna hiyo...’, ‘so that was’ (huyo alikuwa) Mwalimu,” anasema. 

Anasema usomi wa Mwalimu Nyerere, pamoja na kuwa mtu mwenye akili sana, ilimsaidia kuwa mtu wa aina hiyo. 

“Alisoma chuo kikuu kilichopo Scotland, nadhani kilimsaidia sana, acha tu alikuwa na akili za kuzaliwa, lakini pia za kunolewa zilichanganyika zikafanya kitu kizuri. Kwa hiyo Mwalimu alikuwa mtu mwenye huruma sana, vitu vyote alikuwa anaangalia hivyo,” anasema. 

Pili, anasema Mwalimu Nyerere alikuwa anapenda sana familia yake na katika matumizi ya fedha alikuwa si mtu wa matumizi mabaya kuanzia kuvaa kwake. 

“Katika kuvaa kwake nadhani Watanzania wote watakubaliana na mimi, ni mara chache ulimkuta Mwalimu amevaa tai, ‘otherwise’ Vinginevyo, alikuwa akivaa ‘duara’ yake (mashati ya Chuo En lai). 

“Ile, Mwalimu alikuwa anapenda sana familia yake lakini lazima nikubali mara nyingine madaraka ya nchi yalimfanya ayashughulikie mno kushinda wajibu wake kwa familia,” anaeleza. 

“Mimi nafikiri kuna wakati watoto wa Mwalimu walitaka mapenzi ya baba yao, lakini hawakupata ya kutosha, kutokana na majukumu ya kitaifa aliyokuwa nayo Mwalimu,” anasema. 

Anabainisha, alikuwa mtu mwenye malengo na kwamba alipokwenda Umoja wa Mataifa, alionesha kwanini anataka uhuru wa Afrika. 

“Desemba 12, 1962 alisema kwenye Umoja wa Mataifa kwamba, Tanzania hatuwezi kufurahia uhuru wetu kikamilifu hadi Bara la Afrika liwe huru. Uhuru wa Afrika kwa asilimia kubwa ilikuwa ni nguvu ya Mwalimu.

 “Mwaka 1963 OAU ilipozaliwa, Mwalimu alikwenda Addis Ababa kuhudhuria kuzaliwa kwa OAU na ndipo alikwenda kuweka azimio OAU tusikubali uhuru wa nchi zetu umekamilika hadi Bara zima la Afrika liwe huru.

 “Na hapo ndipo likapitishwa azimio la kuunda Kamati ya Ukombozi ya Bara la Afrika, Mwalimu akasema tukiunda makao makuu yaleteni kwangu, ndio maana yakawa Tanzania,” anasimulia.

 Hapo anarejea kumbukumbu, Mkuu wa kwanza wa kamati hiyo, alikokuwa ni Sebastian Chale kutoka Songea na baadae akaja George Magombe na Hashim Mbita, alikuwa wa mwisho.

 “Kamati hii Mwalimu alitaka Tanzania tuitumie kama blanketi na ilikuwa viongozi wa Afrika wakikaa wakisema uhuru wa Afrika na kwamba watakavyosaidia mapinduzi, mtu anasema kabisa anatokwa hadi na jasho.

“Lakini ukiwaambia kulipa kwenye kamati hawawezi, wanasema maneno makali, sisi Tanzania tunasema sawa, sasa sisi hapo hapo ndio tunajificha na ukali wote tunaupeleka kuwa Bara la Afrika linasema na ilitusaidia sana,” anasimulia.

Anakumbuka Samora (Machel) alivyomfuata Mwalimu Nyerere akimwambia kuna watu wake porini anaomba kwa njia yoyote apelekewe magunia 10,000 ya mahindi na iliwezekana kimya kimya ndani ya wiki mbili.

 AONANA NA AMIN

 Anaisimulia Nipashe, kitu ambacho hatokisahau kwa kiongozi huyo (Mwalimu Nyerere) ni wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, alimtuma kwenda kukutana na Idi Amini, kujaribu kupata suluhu kuwaokoa wanafunzi wa Kitanzania katika Chuo Kikuu cha Makerere na Chuo cha Mafunzo ya Urubani cha Soroti, Uganda, ambao walikuwa wamewekwa kizuizini na kuwapo tishio la kuuawa.

 “Kutokana na habari za siri, tulisikia Amin anataka kuwakamata wale watoto awe anawachinja kwa ajili ya kumtishia Nyerere. Hivyo hivyo, tukawa na hakika kama hatutafanya njia ya kuwaokoa watachinjwa.

 “Mwalimu akaniambia, lazima uende na uhakikishe wanafunzi wetu wanatoka salama,” anasema na jukumu, alilokuwa amepewa ni kuomba Amin awaachie wanafunzi waliokuwa wanashikiliwa.

 Kwa mujibu wa Malecela, uamuzi wa kwenda Uganda kuonana na Amin ulitaka ujasiri na aliweka rehani maisha, yake kwa kuwa Amin alikuwa mtu ambaye angeweza kufanya lolote na wakati wowote, bila kujali wala kuhofia chochote.

 Anasimulia katika mazungumzo yao na Amin, alimtamkia Tanzania chini ya Mwalimu Nyerere, ilikuwa inapingana na utawala wake, lakini Malecela akamjibu ‘serikali ya Tanzania haikuwa na tatizo naye kabisa.’

 Kutokana na jibu hilo, Amin aliagiza apelekewe gari ili amwendeshe Malecela mitaa mbalimbali ya Kampala. Hapo Malecela. Anasimulia: “Gari aliloletewa Amin alipoliwasha halikuwaka.

 “Ikabidi iletwe jingine haraka na Amin inaendesha nikiwa nimeketi upande wa abiria. Tupo wawili tu, hatukuwa na ulinzi alitaka kunionyesha jinsi anavyopendwa Uganda.

 “Tulipofika sokoni Nakasero Kampala, Amin aliegesha gari na watu walipomwona walianza kumshangilia. Amin, akanitambulisha akasema: "Mmeona? Mimi sina tatizo na Nyerere wala Tanzania. Huyu hapa ni Waziri wa Nyerere, amekuja kututembelea. 

 “Na mimi nimemleta mumuone muone sina tatizo na Nyerere. Kuanzia leo nisisikie Mtanzania yeyote anasumbuliwa hapa Uganda. Sisi na Wtanzania ni ndugu."

 Anasema walipotoka sokoni, walizunguka maeneo mengine ambayo Amin aliendelea kumtambulisha Malecela na kusisitiza undugu wa Tanzania na Uganda.

 “Wakati anafanya mazungumzo na Amin, upande wa pili kulikuwa na operesheni ya kuwatorosha wanafunzi waliokuwa wanasoma Makerere na Soroti. 

 “Wale wa Makerere wote walirejeshwa Tanzania salama. Shida ilikuwa kwa wale wa Soroti walikuwa 21 wao walisema wasingeondoka, kwa sababu walibakiza mwezi mmoja ili kufanya mitihani yao ya mwisho ya kumaliza masomo ya urubani,” anasema.

  Soroti ni chuo kichotoa mafunzo ya urubani na watalaamu wengi wa Afrika Mashariki walisoma huko.

 Anasema aliporejea Tanzania na baada ya kubainika wanafunzi wa Kitanzania waliokuwa Makerere 400 tayari walishatoroshwa, wale 21 wa Soroti wote waliuawa na askari wa Amin.

  NYERERE NA KAWAWA

Anasimulia Mwalimu Nyerere alikuwa mwanasiasa na Watanzania walimuelewa, lakini wakati kulikuwapo propaganda za kuigawa nchi kidini na vilizuka vyama vitatu (zama za kugombea uhuru).

 “Kama Watanzania tusingekuwa makini tungegawanyika, sasa wakati huo Kawawa alikuwa mtu wa chama cha wafanyakazi (TFL), mtu wa kuitisha migomo ya wafanyakazi na alikuwa vizuri. 

 “Ili tusiingie kwenye migawanyiko ya kidini Kawawa aliiona hiyo na Nyerere akaiona wakawa pamoja kwa hiyo vyama vya wafanyakazi vyote vikawa wao na TANU ni kitu kimoja,” anasema.

 Anafafanua Kawawa, alipoungana na Nyerere, alikuwa na nguvu ya wafanyakazi (chama cha TFL) na walifanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.

 “Lazima nikubali kitu kimoja, Kawawa akawa ni mtu anayeheshimu usomi wa Nyerere na ujuzi wa Nyerere. Walipoungana na walivyofanya, ndio hadi sasa Tanzania tupo tulipo na Tanzania ya leo ukitaka watu wakuchukie kweli kweli sema habari ya dini,”anasema.

 SIRI YA MAAZIMIO

Anasema Mwalimu Nyerere, kila kitu alichotaka kuanzisha kipya alianzia kwenye chama kujadili na kuja na kitu kama kwenye Azimio la Arusha, Azimio la Iringa (Siasa ni Kilimo), Azimio la Musoma (Elimu) yenye kuwapa Watanzania matumaini.

 “Azimio la Arusha liliitisha watu na alikwenda kufanya kwenye ‘kakibanda’ kadogo na wengi walifikiri tukifika pale tutashindwa, kwamba tutapata migomo watu wataandamana, walidhani ni mwisho wa TANU.

 “Lakini kilipotokea mabenki kutaifishwa mimi niliona watu wa serikali wanaingia NBC, watu wapo nje tu wanafurahia eeehe eehee! na ilikuwa kila sehemu matawi yalipo,”anasema.

 Anafafanua kuwa baada ya Arusha, likaja Azimio la Iringa na lilizalisha suala la ‘Siasa ni Kilimo’ na wakulima majeuri walikuwa Iringa na Mbeya.

 “Azimio lilitaka kuonyesha Watanzania wafanye nini kwenye kilimo. Lilizungumzia ‘aspects’ za mazao kwamba yalimwe na wapi na masoko yake yawe wapi. Mwalimu alitaka kuwaondoa Watanzania kwenye mawazo ya siasa na alitaka kuwapeleka kwenye kilimo,” anasema.

 Mzee Malecela anasema baada ya azimio hilo, alikuja na linalohusu elimu na lilifanyika Musoma, akiendelea: “Mambo mengi yanayotekelezwa sasa ni ya Azimio la Musoma la Elimu, kwa kweli utaona miongozo ya namna ya kujenga Tanzania bora na inayojali maskini inatokana na chama tawala,” anasema.

 OPERESHENI VIJIJI

 Anasimulia siasa za Tanzania zinatokana na miongozo iliyotokana na Mwalimu Nyerere kwa kila sekta kama elimu, kilimo na afya, pia ana ufafanuzi wake: 

 “Kikubwa alichofanya Mwalimu Nyerere kukumbukwa ni alipokuwa anaendesha Operesheni Vijiji vya Ujamaa, alikuwa Chamwino kwenye ‘mbuyu wake’ bado upo na kivuli chake…alikuwa anasema hivi ‘John (Malecela) kapeti likiwa chini unaliona zuri, hebu liinue ndani utakuta uchafu mwingi.

 “Akasema vijiji vyetu tuvirundike pamoja, watu waliokuwa wanapinga vijiji vya ujamaa na watu walikuwa wametawanyika lakini vilipoanzishwa vijiji ikawa rahisi kushirikishana shughuli za kijamii.

 “ Wapinzani wakaidaka wakasema ooho watu wanakufa, kwa kweli tulipofanya vijiji tulilifungua kapeti ili tuondoe taka za chini,”anasema.

 Anabainisha kwenye vijiji wamepeleka zahanati, shule za msingi, maji safi na hayo yote yametokana na siasa ya operesheni vijiji.

 “Mawazo ya Mwalimu hadi leo bado ni mwongozo na mimi nitasikitika sana kama tutafika mahali tusichukue mawazo ya Mwalimu ni msingi wa maendeleo Tanzania,” anasema.

 DODOMA MAKAO MAKUU

 Anasema Mwalimu Nyerere alipokuja na Azimio la Kuhamia Dodoma, lililetwa na Paul Bomani, kwa kauli: “Watu wa Mwanza tunatoka mwisho wa reli hadi mwisho, Mwanza hadi Dar es Salaam.

 “Kwanini tusitafute makao makuu mahali kwamba wenzetu wa Dar es salaam watakuja na sisi wa Mwanza tutakuja ndio ikawa Dodoma.”

anasema.

 Anabainisha Mwalimu Nyerere hakushindwa kuwezesha kuhamia Dodoma, lakini wakati akiwa katika mkakati huo ndio nchi ikakumbwa na vita vya Idd Amin na ilichukua uchumi kwa kiasi kikubwa.

 ·      Kesho, fuatilia maisha yake Mzee Malecela, alikotokea na mengi aliyofanya kufikia leo, umri miaka 90.