Kinamama watakiwa kuwekeza katika malezi, makuzi ya mtoto

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:34 PM Oct 14 2024
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaid Khamis ( katikati) akiwa na wanachama wa mum's club Jubilee Health Insuatance.
Picha: Mpigapicha Wetu
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaid Khamis ( katikati) akiwa na wanachama wa mum's club Jubilee Health Insuatance.

NAIBU Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaid Khamis amewataka kinamama kuwekeza katika malezi na makuzi ya awali ya mtoto ili kupata jamii yenye afya ya mwili, akili na kiroho.

Alitoa wito huo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam katika hafla ya Jubilee ya kinamama yenye lengo la kusherehekea na kutoa elimu kwa wanawake ili kuwasaidia kuboresha malezi na makuzi ya watoto.

Alisema serikali inatambua na kuheshimu mchango unaotolewa na sekta binafsi katika usimamizi na utekelezaji wa afua mbalimbali hususani utoaji wa elimu umma kuhusu malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.

"Nimefarijika kuona ushirikiano mzuri uliopo kati ya Kampuni ya Jubilee Health Insuarance na wananchi ambao unaishi kwa vitendo kwani tumeona kuna ushirikishaji jamii katika utoaji elimu ya malezi na makuzi ya mtoto ambayo inatolewa kwa wanawake wanachama na wasio wanachama," alisema.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jubilee Health Insuarance, Hellena Mzena alisema klabu hiyo ina wanachama zaidi ya 1,000 na ilianzishwa mwaka 2022.

Alisema tatizo la uzazi nchini ni kubwa, kwamba kina mama 104 wanafariki dunia wakati wa kujifungua kati ya kinamama 1,000.

Alisema klabu yao inashirikiana na serikali katika kupambana na tatizo hilo ikiwemo kutoa elimu sahihi ya uzazi na malezi kwa kinamama kabla na baada ya kujifungua.