Samia aahidi kununua vifaa vya kisasa utafiti wa madini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:45 AM Oct 14 2024
Samia aahidi kununua vifaa vya kisasa utafiti wa madini

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema ni asilimia 16 tu ya madini yote yanayopatikana nchini na kuuzwa ambayo yamefanyiwa utafiti.

Kutokana na hali hiyo, amesema serikali imejipanga kuwekeza katika ununuzi wa vifaa, zikiwamo helkopta, vitakavyosaidia kufanya utafiti nchi nzima kutambua maeneo yenye madini na kiwango chake.

Rais Samia alitoa kauli hiyo jana, mkoani Geita wakati akifunga maonesho ya saba ya teknolojia ya madini na kueleza kuwa baada ya uwekezaji huo, serikali itakuwa na uwezo wa kwenda nje na kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo.

"Hapo tutakuwa na uhakika wa kiasi gani cha madini kimo ndani ya nchi, hivyo tumeongeza fedha nyingi kwa ajili ya kufanya utafiti, ili tuwe na takwimu nzuri na za uhakika katika rasilimali yetu hii ya madini," alisema.

Rais alisema uwekezaji huo wa serikali utaleta matokeo mazuri kama ilivyokusudiwa na kuwa tayari yameanza kuonekana katika mchango wa Pato la Taifa. Kwa mwaka 2023, mchango wake ulikuwa asilimia tisa kutoka asilimia 7.2 huku lengo likiwa ni kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Alisema sekta hiyo inaongoza kwa kuliingizia taifa fedha za kigeni na kuwa kwa mwaka 2023 iliingiza asilimia 56 ya fedha zote za kigeni, hivyo kuahidi kuwa serikali itaendelea kuipa kipaumbele kwa kuwainua wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa sambamba na kuwa karibu nao.

Alisema ongezeko hilo limetokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali, ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji pamoja na upatikanaji teknolojia ambako kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), serikali imefanya ununuzi wa mitambo mikubwa 15 ya uchorongaji miamba.

"Mitambo mitano imeshafika nchini na 10 ipo njiani inakuja, ili kuwarahisishia wachimbaji kufanya kazi kwa uhakika na kuwaepusha na hasara," alisema.

Rais pia alisema mitambo hiyo itakapofika itatawanywa katika maeneo yote ya uchimbaji, akimwagiza waziri kutenga mitambo miwili mahususi kwa ajili ya wachimbaji vijana na mtambo mmoja kwa wachimbaji wanawake.

Pia alisema serikali imetenga Sh. bilioni 200 kama dhamana ya mikopo, ili kuwawezesha wanunuzi wa madini kukopa na kufanya kazi zao vizuri.

"Vivyo hivyo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeweka Sh. trilioni moja kwa ajili ya ununuzi wa dhahabu, hivyo  yote hiyo ni mipango ya kuhakikisha tunakuza madini na kwa wakati huo tunabaki na akiba ya dhahabu kama dhamana ya utajiri wetu kwa siku zijazo," alisema.

Rais alisema masoko ya madini yaliyosogezwa kila mkoa pamoja na vituo vya kununulia madini katika maeneo yanakochimbwa madini, sasa kukiwa na masoko 44 katika mikoa yote na vituo 103 vya kununulia madini, yamesaidia kuwapo mzunguko mzuri wa biashara.

"Kwa mwaka 2023/24, madini yenye thamani ya zaidi ya Sh. trilioni mbili yaliuzwa kupitia masoko ya madini na kuwezesha serikali kukusanya kiasi cha Sh. bilioni 180 kutokana na masoko hayo mbali na mapato mengine yanayokusanywa na wizara," alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema serikali imefuta leseni zaidi ya 2,000 zilizokuwa zimehodhiwa kwa muda mrefu, wakiwamo wawekezaji wazawa waliokuwa waliohodhi leseni zenye ukubwa ya ekari zaidi milioni 13, ambazo watagawiwa wachimbaji wadogo kwa kuweka kipaumbele kwa vijana na wanawake.

Mavunde alisema Wizara ya Madini ina mpango wa MBT unaolenga kuwafikia vijana na wanawake.

"Sh. bilioni 231 zimetengwa na kuelekezwa kwenye Taasisi ya Utafiti wa Madini (GST) na kwamba maabara kubwa mbili; moja itajengwa Dodoma na maabara za kanda; moja itajengwa Mkoa wa Geita kwa ajili kuwasaidia wachimbaji kupima sampuli," alisema Mavunde.

Rais wa Shirikisho la vya Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania, John Bina, alimwomba Rais Samia kuweka msamaha wa kodi, kwa vifaa vya uchimbaji madini ya dhahabu vinavyonunuliwa na wachimbaji wadogo, ili kuwawezesha kuchimba madini kisasa.

Alisema kupitia kikao chao kilichofanyika Dodoma hivi karibuni, walikubaliana wachimbaji wadogo wa madini na wafanyabiashara kuizuia BoT asilimia 20  ya madini ya dhahabu, hivyo kutaka benki hiyo iwe imara kuviwezesha viwanda vya kusafisha madini vipate mtaji, ili zifanye kazi kwa uhakika.

Mkuu wa Mkoa  wa Geita, Martine Shigela, alisema maonesho hayo yanakuwa kila mwaka na kwamba mwaka jana, walikuwa na washiriki 350 kutoka ndani na nje na kwa mwaka huu washiriki  wameongezeka na kufikia 856.

"Sh. bilioni saba zimetengwa na serikali kupeleka umeme kwenye maeneo ya wachimbaji wadogo ambao wamezalisha zaidi ya kilo 16,262 zenye mauzo ya Sh. trilioni 2.2," alisema Shigella.

Imeandaliwa na Alphonce Kabilondo (GEITA), Neema Emmanuel na Vitus Audax (MWANZA).