UCHAGUZI MITAA: CHADEMA yalia wanafunzi kuandikishwa, waziri ajibu

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:34 PM Oct 16 2024
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetaja kasoro 18 mbalimbali zilizoko kwenye uandikishaji wa wapigakura kwenye Daftari la Wakazi ulioanza Oktoba 11, mwaka huu.

Awali, Oktoba 13, mwaka huu, Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, alitaja kasoro tano ambazo zimetajwa pia na CHADEMA ikiwamo kuandikishwa kwa watoto ambao hawajatimiza miaka 18.

Wakati malalamiko hayo yakitolewa, jana Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, alijibu hoja hizo kwamba kila Mtanzania mwenye umri wa miaka 18 anaandikishwa bila kujali ni mwanafunzi au la.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kutaja kasoro 18 ambazo wamezibaini katika uandikishaji.

Alitaja kasoro ya kwanza kuwa vituo vya uandikishwaji kuwekwa kwenye majengo au nyumbani kwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema jambo hilo limetokea katika maeneo mbalimbali kama Korin Kusini, Kitongoji cha Rau Jimbo la Moshi Vijijini.

Kasoro ya pili ni waandikishaji kuruka namba kwenye madaftari ya kuandikisha wapigakura, wakiamini kuwa lengo la kufanya hivyo ni baadaye kuja kuingiza majina feki. Alitaja kasoro ya tatu kuwa ni kuandikishwa kwa wanafunzi ambao hawajafikisha miaka 18 na kuendelea.

Mrema alitaja kasoro ya nne kuwa ni baadhi ya waandikishaji kuwa wanachama wa CCM na tano ni wenyeviti wa mitaa, vijiji na vitongoji ambao wako madarakani kuwa sehemu ya mawakala. Kasoro ya sita ni viongozi na wanachama wa CCM kupeleka majina ya waandikishwaji.

Alitaja jambo la saba kuwa ni vituo vya uandikishwaji kuwekwa kwenye kambi ya vyombo vya ulinzi na usalama, nane ni uandikishaji kuanza kabla ya muda uliowekwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi na tisa ni baadhi ya wakuu wa wilaya kuingilia shughuli ya uandikishaji.

Jambo la 10, kwa mujibu wa Mrema, ni waandikishaji kuacha vituo na kwenda kuandikisha mitaani na kasoro ya 11 ni mawakala wa CHADEMA kutoruhusiwa kuingia kwenye vituo vya uandikishaji. Pia alisema kuna uandikishaji wa majina hewa na  waandikishaji kuongeza majina ya watu ambao hawakufika kwenye kituo na pia  mawakala kuzuiwa kuondoka na idadi ya watu walioandikishwa.

Jambo la 15, alisema ni watu kuandikishwa nje ya kituo na 16 ni kukamatwa kwa wanachama na viongozi wa CHADEMA na Jeshi la Polisi.

Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Songwe, Isakwisa Lupembe, alisema katika Jimbo la Tunduma, watoto wanachukuliwa shuleni kwenda kuandikishwa, hoja iliyopingwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Tunduma, Mariam Chaurembo, ambaye ni msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo.

KAULI YA MCHENGERWA

Mchengerwa alisema hatua ya uandikishaji wa wananchi katika daftari la wakazi kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa umefikia asilimia 45 huku asilimia 55 hawajajiandikisha.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza, alisema pamoja na mambo mengine, wizara hiyo imehakikisha inatoa elimu kwanza kuondoa mkanganyiko wa wananchi kuchanganya kati ya uandikishwaji katika Daftari la Kudumu la Mpigakura na Daftari la Wakazi la Serikali za Mitaa.

“Tukiri kuwa suala hili bado linahitaji kutolewa elimu kwani mchakato wa uchaguzi ni wa mwaka mzima na haufanywi tu kwenye wizara hiyo bali ni wa kila Mtanzania aliyefikisha umri wa miaka 18 pamoja na vyama vyote vya kisiasa,” alisema.

Pia alisema jukumu hilo linavihusu pia vyama vya kisiasa, hivyo si vyema kulalamika kuwa elimu haijapelekwa bali na wao wanatakiwa kuhakikisha wanatoa elimu kwa wanachama wao.

Alisema elimu inaendelea kutolewa kupitia wakuu wa mikoa, wilaya, vyombo vya habari pamoja na wakurugenzi katika halmashauri kupitia hamasa na ufafanuzi wa hoja mbalimbali zinazoibuka pamoja na taasisi zaidi ya 83 zilizoomba kutoa elimu hiyo katika maeneo yote nchini.

“Tumesikia kuwa kuna uandikishwaji wa watoto ambao hawajakidhi vigezo bado hatujapata uthibitisho wa masuala hayo lakini nitoe maelekezo kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuhakikisha wanafuata sheria, taratibu na kanuni zilizotolewa,” alisema Mchengerwa.

Kuhusu wasimamizi wa vituo kukataa kutoa takwimu, alisema suala hilo lipo kwa mujibu wa sheria za uchaguzi na kuwa jukumu lao ni kuhakikisha wanaandika kila mwananchi mwenye vigezo huku mawakala wakiwa na jukumu la kuwatambua waliokwenda kujiandikisha ili kujua kama ni halali.

Alisema baada ya hatua hiyo, kitakachofuata ni kuwaorodhesha wote waliojiandikisha na kubandika katika maeneo husika, ili kubaini kasoro na kuzifanyiwa marekebisho.

Waziri alisema kanuni hizo zimeandaliwa na kupitishwa kwa ushirikiano na vyama vyote 19, hivyo viongozi wa vyama wanatakiwa kutambua ni namna gani ya kushughulika na mazingira wanayobaini kuwa yana kasoro.

Kuhusu vituo bandia, alisema hakuna suala kama hilo na kuwa vituo vyote vinavyotumika vipo kisheria ambavyo ni 80,812 kati ya mitaa, vijiji na vitongoji 68,543.

Alisema pamoja na mambo mengine ipo mikoa iliyofanya vyema kwa kipindi hicho cha siku nne kwa kuvuka asilimia 54.2 ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Tanga, Ruvuma, Njombe, Songwe, Lindi na Iringa.

Kadhalika alitaja mikoa ambayo bado ipo nyuma kuwa ni pamoja na Katavi, Kilimanjaro, Geita, Kigoma na Manyara huku mikoa yenye watu wengi ambayo bado iko chini ya asilimia 40 kama zilivyoainishwa kwenye mabano Dar es Salaam (35.3), Mwanza (34.2), Morogoro (37.9), Dodoma (38.5), Tabora (27.7) na Kagera (34.8).

Imeandikwa na Vitus Audax (MWANZA), Jenipher Gilla (DAR) na Moses Ng'wat (TUNDUMA)