MAZUNGUMZO MAALUMU-2 KAMANDA MSSIKA; Mkasa alipotuhumiwa anataka kununua u-IGP

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 12:46 PM Oct 16 2024
news
Picha:Nipashe Digital
Kamanda mstaafu Abdallah Mssika, akiwa katika ofisi za The Guardian.

Jana katika ufafanuzi wake alipozungumza na Nipashe, alieleza safari ya maisha yake, akianzia kwenye ufundi gereji hadi kushika nafasi mbalimbali ndani ya Jeshi la Polisi, ikiwamo kuwa Msaidizi wa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP). Endelea...

---

KAMANDA Mssika anasimulia matukio binafsi ambayo hawezi kuyasahau maishani mwake kwa miaka 40 aliyotumikia Jeshi la Polisi kuwa ni pamoja kutuhumiwa kutaka kununua ateuliwe kushika nafasi ya IGP mwezi Januari 2006.

Anaeleza kwa kina matukio manne akikumbuka pia, shambulio la bomu katika Ubalozi wa Marekani nchini.

"Nikiwa Kamanda wa Polisi Shinyanga, matapeli kutoka Dar es Salaam waliwasiliana na mimi kwa njia ya simu kwa kunipongeza kuwa ni miongoni mwa baadhi ya makamanda waliomo katika orodha ya kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete katika nafasi ya IGP kwa vile IGP aliyekuwapo kwa wakati ule alikuwa anastaafu," anasimulia.

Kamanda Mssika anasema mwakilishi wa matapeli hao aliyekuwa anawasiliana naye, alimjulisha kwamba wao ndio walikuwa katika kamati maalum ya kuteua na kwamba kati ya makamanda waliokuwamo katika orodha ya mwisho, yeye (Mssika) alikuwa anaongoza kwa sifa za juu.

"Hakuishia hapo, akaniambia kwa vile kamati yao imetakiwa kuwasilisha jina langu kwa Mheshimiwa Rais mara tu atakapomaliza kuzungumza na baraza lake la mawaziri aliokwishawateua na mhasibu wa Ikulu yuko pamoja katika msafara wa Mheshimiwa Rais, hivyo, akanitaka nitume fedha za kujikimu haraka ili wakamilishe kazi yangu. 

"Nilitambua mara moja ni matapeli, nikikumbuka tukio la matapeli kutaka kumtapeli Mkuu wa Wilaya ya Lindi (wakati huo) Fatuma Mikidadi, nikiwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi mwaka 2003," anasimulia.

Kamanda Mssika anasema kuwa katika tukio la mkuu wa wilaya huyo, walimlaghai na kumtisha kwamba alikuwa ni mmoja wa wakuu wa wilaya waliokuwa katika orodha ya wenye sifa ya kuteuliwa na Rais Benjamin Mkapa kuwa wakuu wa mikoa.

"Walimtisha kuwa kinachomwangusha ni 'kiongozi aliyejilimbikizia mali isivyo halali' na kamati yao iliyoundwa kumshauri Rais watapendekeza afukuzwe kazi na kukabidhiwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa hatua zaidi.

"Wakamtaka awatumie haraka Sh. milioni tatu kwa njia ya huduma ya Posta Western Union, huduma ambayo hata hivyo wakati huo ilikuwa haijafika Lindi. Walikamatwa wote," anasimulia.

Kutokana na tukio hilo, Kamanda Mssika anasema alipopigiwa simu kwamba yumo katika orodha ya wanaopendekezwa kwa nafasi ya IGP, alibaini haraka "hizo ni mbinu za matapeli" kutokana na uzoefu wake kazini.

"Yaani kamanda nitoe fedha kuhonga wasaidizi wa Rais na Amir Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ili niteuliwe kuwa IGP!" Kamanda Mssika anamtaka kwa msisitizo na hisia.

Anasema kitendo cha watu kujiamini mpaka kufikia kujenga ujasiri wa kuwafuata makamanda kadhaa wa polisi, yeye akiwa ni miongoni mwao ili kuwatapeli, aliona ni uhalifu mkubwa na wana uwezo wa kufanya chochote, ikiwa ni pamoja na udhalilishaji taasisi nyeti kama Jeshi la Polisi.

"Nikiwa Shinyanga, matapeli waliowasiliana na mimi, nikawaaminisha wanachofanya ni sahihi, lengo waamini kwamba wamenipata na kuwaaminisha wanachofanya ni sahihi na msaada wao utakuwa na faida kwangu.

"Ndipo nilipowasiliana na Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam (ZCO) na kumweleza picha kamili na hatua nilizochukua kuhakikisha wanakamatwa Dar es Salaam waliko.

"Nilimweleza nilishaingiza benki (anaitaja) Sh. 350,000 katika akaunti niliyopewa na matapeli kwa ahadi kiasi kingine cha fedha kilichosalia nitawakabidhi pale Uwanja wa Ndege Dar es Salaam siku iliyokuwa inafuata kwa sababu nilikuwa safarini kutoka Shinyanga kwenda Arusha," anasimulia.

Kamanda Mssika anasema walikubaliana makachero wawapo uwanja wa ndege ili atakapotua wawakamate kwa mbinu waliyokubaliana.

Anasema kuwa baada ya kutua na kutoka nje ya uwanja wa ndege, upande wa abiria wanaowasili, awali hakuona mtu yeyote akimfuata; si matapeli wala kachero.

Anasema kuwa baadaye wakati anaangaza macho huku na huko, alimwona kachero mwandamizi (bila kumtaja jina) aliyekuwa anaongoza timu ya makachero katika ukamataji huo ambaye alimweleza kwamba tayari wameshawakamata matapeli hao.

"Akaniambia ‘Afande Mssika, pole kwa safari, wale matapeli tumeshawakamata'. Nilihoji mmewakamataje? Akanijibu 'hapana, mazingira ya mipango ya awali yalibadilika baada ya matapeli wale kuonekana wakiwa airport (uwanja wa ndege)'.

"Hivyo, ofisa kiongozi wa timu ya ukamataji akanifafanulia kwamba, 'tulivyowaona tu afande, tuliwatambua mara moja kuwa ndio timu yenyewe ya utapeli wa aina hiyo', tukajua bila shaka kwamba ndio wenyewe'.

"Akaniambia wamekamatwa watuhumiwa wanne na tayari walikuwa wamepelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar kwa mahojiano na uchunguzi zaidi, lakini washirika wenzao wengine walitoroka kabla hawajakamatwa," anasimulia.

Kamanda Mssika anasema wakati wa harakati za kuwakamata matapeli hao, alikuwa amehamishwa kutoka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga kwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha na amri ilikuwa imeshatolewa.

"Wakati nikisubiri asubuhi kukuche ili niende kwa ZCO na baadaye Makao Makuu ya Polisi, asubuhi magazeti yakawa yameandika 'RPC atapeliwa kwa ahadi ya kuwa IGP, aliambiwa mipango imeiva naye akaingia, akatoa Sh. milioni 2.5'.

"Sijakwenda kwa ZCO wala kuandika maelezo yangu, tayari mambo yamekwenda mbali. Hata kwenda Makao Makuu ya Polisi kumwona IGP kumweleza niko safarini kuelekea Arusha, safari haikuwapo kwa sababu uhamisho ukawa umefutwa siku hiyo hiyo.

"Ninachofikiria mpaka sasa na ndicho ninachoamini, kilichofuata baada ya hapo ni mimi badala ya kwenda Arusha nikapelekwa kuwa Mkuu wa Utawala na Fedha Kanda Maalum ya Dar es Salaam nikiwa chini ya Kamishna Alfred Tibaigana baada ya (kitengo hicho) kuundwa kwa mara ya kwanza na Rais Kikwete," anasimulia.

Kamanda Mssika anasema hakukaa muda katika kitengo hicho, akapelekwa kuwa Kamanda Polisi Mkoa wa Kagera kuchukua nafasi ya Kamanda (Venance) Tossi aliyehamishiwa Makao Makuu kwa kazi nyingine na baadaye akateuliwa kuwa Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini.

"Kamanda mwenye tamaa ya kuwa IGP kwa kuhonga, inawezekanaje huyo huyo kupewa majukumu hayo kuanzisha Kanda Maalum Dar es Salaam, Tibaigana akiwa hayupo anakaimu majukumu hayo na kwenda Kagera kuwa kamanda na hatimaye kuwakilisha Jeshi la Polisi kama msemaji?" anahoji.

Kamanda Mssika anasema taasisi mbalimbali zilizomhoji na kwa maelezo aliyotoa, yalionekana na mamlaka za kiuchunguzi ndio sahihi kuliko yale ya awali yaliyosambazwa na vyombo vya habari.

"Sikupata mrejesho kama maelezo yangu ndio sahihi isipokuwa kwa vitendo kwa kuwajibika kupewa nafasi mpaka hatimaye kustaafu, nikatunukiwa medali nyingine na nishani ya utumishi uliotukuka.

"Mpaka sasa sifahamu waliofanya hivyo ni nani, zaidi ya waliokamatwa. Siwezi kujua ni nani? Namna gani au wapi ilifanyika? Lakini hatimaye nilikuja kuaminika," anasema.

Mbali na medali na nishani Kamanda Mssika aliaminika hadi kuwa mwalimu wa Chuo cha Polisi Kurasini (Dar es Salaam) kuanzia mwaka 1990-1996, akifundisha makachero masomo ya Upepelezi wa Makosa ya Jinai, yakijumuishwa pia matukio ya makosa ya wizi wa kalamu/kughushi.

"Ualimu ambao mafunzo yangu ya kuwa CID nilipata Uingereza katika Chuo cha Detective Training School kilichoko mji wa Wakefield, West Yorkshire England kwa ufadhili wa British Council. Tulikuwa na wenzangu 10 na ilikuwa mwaka 1990.

"Lengo la mafunzo haya ni baada ya serikali kupanga kujenga chuo kikuu cha makachero kimataifa CID  Ukanda wa Kusini mwa Afrika ambacho kingekuwa Dodoma.

"Baada ya mafunzo, nikapelekwa Chuo cha Polisi Kurasini kufundisha walimu wa walimu ambao ni timu ya awali. Nilikaa chuoni miaka sita na baadaye kupelekwa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kuwa Msaidizi Aid de Camp (ADC) wa IGP Omar Mahita.

AJALI YA HELIKOPTA

"Tukio lingine ninalokumbuka ni ajali ya helikopta iliyotokea Nachingwea, tukiwa na IGP akizunguka kukagua maeneo yale. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi alifariki dunia. Hili ni tukio la kukumbuka," anasema.

SHAMBULIZI UBALOZINI

Kamanda Mssika anasimulia tukio lingine ambalo hatosahau ni baada ya kutolewa kwa IGP na kupelekwa Kituo cha Polisi Oysterbay kuwa OCD.

Katika utekelezaji majukumu hayo mapya, anasema kulitokea shambulizi la bomu katika Ubalozi wa Marekani nchini.

"Dakika 20 au 30 wakati tukio linatokea siku hiyo ilikuwa ni paredi ya OCD ambapo huwa na mkusanyiko wa askari wengi. Wakati linatokea tulikuwa tumemaliza ukaguzi wa paredi, askari wanaingia katika magari kwenda doria.

"Awali tulidhani mlipuko huo ulitokea bandarini, lakini kupitia askari waliokuwa pointi ya Kenyatta wakati huo, walitujulisha kupitia radio call kuwa ni ubalozini.

"Tulitoka moja kwa moja kwenda eneo la tukio, tukadhibiti eneo vizuri. Msaada tuliotoa uliwezesha vielelezo muhimu kupatikana kwa haraka," anasema.

Kamanda Mssika anataja matukio mengine yaliyokuwa yanatokea wakati huo ni migomo ya wanafunzi wa chuo kikuu ambayo walikuwa wanayashughulikia kwa utaratibu anaotaja "mzuri ambao ulifanikisha kurejesha utulivu".

*ITAENDELEA KESHO