TRA yafungua ofisi maalum kwa walipakodi wakubwa

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 02:38 PM Oct 16 2024

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa mamlaka hiyo pamoja na waandishi wa habari (hawapo pichani), jijini Dar es Salaam kabla ya kufungua ofisi maalum ya walipa kodi binafsi.
Picha: Grace Gurisha
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa mamlaka hiyo pamoja na waandishi wa habari (hawapo pichani), jijini Dar es Salaam kabla ya kufungua ofisi maalum ya walipa kodi binafsi.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imefungua ofisi maalum kwa ya walipa kodi binafsi wenye hadhi ya juu ili iweze kuwaaangalia kwa ukaribu na walipe kile wanachostahili kuepuka kupata matatizo badaye, baada ya kufanyiwa ukaguzi.

Aidha, imesema walipa kodi hao ni wamiliki wa kampuni wanaoingiza Sh. bilioni 20 kwa mwaka, wamiliki wa hisa wanaoingiza zaidi ya Sh. bilioni 2.5, viongozi wanaomiliki kampuni na wale wenye ubia kwenye kampuni wanaoingiza Sh. bilioni 20 kwa mwaka.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 16,2024 jijini Dar es Salaam na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda wakati akifungua ofisi hiyo yenye hadhi ya juu iliyopo jengo la Golden Jubilee Tower, amesema lengo ni kuendelea kuimarisha huduma za kikodi kwa walipa kodi.

Aidha, amesema wameanza na walipa kodi 158  ambao mapato yao ni makubwa, wanamiliki kampuni, wameajiri watu na pia  kampuni zao zinalipa kodi na wao wanapaswa kulipa kodi kama waajiriwa wengine.

 "Tumeanza na hawa 158, walipa kodi binafsi wapo 111 wote wameshaitwa hapa na viongozi wa miimili mitatu ya juu wapo 47 , tunawapa huduma bora kwa sababu wanamchango mkubwa tukiwaacha wakakosea kidogo, tutakosa mapato,"amefafanua Mwenda. 

Kwa mujibu wa Kamshna huyo,  lengo ni kuangalia kodi zao wao sio za kampuni zao, kwa hiyo wanahitaji kupata elimu ya kutosha mara kwa mara na pia wanahitaji kuangalia kile wanachostahili walipe.

 "Hii ni uthibitisho kwamba hawa nao wanalipa kodi kama wengine kama mwajiriwa anavyolipa na hawa pia walipe, kanuni yetu ya mfumo nzuri wa kodi inawataka wenye uwezo mkubwa kama hawa walipe kodi inayotakiwa,"amesema na kuongeza:

 "Hizi ndizo sababu za kuwaleta hapa, tunawashukuru sana kwa mchango wanaotoa, nashukrani zetu ni kuwadumia wasipate matatizo ya kutolipa wanachostahili bali walipe wanachostahili."

Pia amesema kuna kundi lingine la viongozi wataenda badae katika ofisi hiyo, ambapo watakuwa wanahudumiwa hapo kutokana na mapato ya shughuli wanazofanya kama ajira na wao wataangaliwa kwa ukaribu na kushauriwa, ili wachangie kile wanachostahili.

"Hawa wanatakiwa kuchangia asilimia 30 ya mapato yao kama anachokipata kwenye shughuli zake, wanakuwa na shughuli nyingi wanaweza wakawa na kampuni, anaweza akawa amewekeza anaweza akawa na biashara nyingine, kwa hiyo mapato yale yote, sasa hivi yatakuwa yanaangaliwa kwa pamoja,"amesema.