Miradi ya Bilioni 8.6 ilikataliwa na Mwenge

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 05:18 PM Oct 16 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Godfrey Mnzava.
Picha: Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan akipokea Mwenge wa Uhuru kutoka kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa, Godfrey Mnzava.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Ridhiwan Kikwete amesema miradi 16 yenye thamani ya Sh. bilioni 8.6 ilikataliwa na Mwenge wa Uhuru baada ya kubainika kuwa na kasoro na kukabidhiwa TAKUKURU kwaajili ya uchunguzi wa kina.


“Kupita mbio hizi miti 150,159,594 imepandwa miradi 1595 yenye thamani ya Sh.trilioni 11 imezinduliwa na kukaguliwa tofauti na 1424 yenye thamani ya Sh.trilioni 5.3 iliyofikiwa mwaka 2023,”amesema  Ridhiwani.

Amesema mwenge huo umekimbizwa kwa zaidi ya km 37,235.62 katika mikoa 31, halmashauri 195 kwa siku 195 ukiongozwa na vijana sita wawili kutoka Zanzibar, Kigoma, Kilimanjaro, Dar es Salaam huku kiongozi wa mbio hizo Godfrey Mzava akitokea mkoani Mwanza.

Jana Mwenge wa Uhuru uliwasili mkoani Kilimanjaro na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu kwaajili ya kuanza rasmi safari ya kupandishwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro leo Oktoba 16,2024.

Safari hiyo imeendelea mapema leo ambako Waziri Ridhiwani amesema Tanzania inapeleka Mwenge wa uhuru juu ya mlima Kilimanjaro, ili kuitangazia dunia kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni imara na pia utaendelea  kulinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Kadhalika, amesema kwa mwaka 2024, Rais Samia Suluhu Hassan ameamuru mwenge wa uhuru upelekwe juu ya Mlima Kilimanjaro baada ya kuhitimisha mbio zake kwa siku 195 na kuwa mbio zake kwa mwaka 2025 zinatarajiwa kuzinduliwa mkoani Pwani na kuhitimishwa mkoani Mbeya.