Makalla: CCM imeridhika uandikishaji wapiga kura

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:26 PM Oct 16 2024
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla akijiandikisha katika daftari la mpiga kura katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa TPDC Kata ya Mikocheni.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla akijiandikisha katika daftari la mpiga kura katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa TPDC Kata ya Mikocheni.

KATIBU wa NEC-Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Amos Makalla amesema CCM imeridhika na zoezi la uandikishaji wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Amesema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokwenda kujiandikisha katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa TPDC Kata ya Mikocheni.

Makalla amesema kuwa CCM imeridhika na jinsi zoezi la uandikishaji linavyoendelea kote nchini, kwamba matumaini ya chama ni wananchi wataitikia wito huo kwa wingi.

“Ni jambo muhimu sana kujitokeza na kujiandikisha, kwani ndilo linaloweka msingi wa maendeleo ya wananchi wetu,” amesema Makalla.

Aidha, amewasihi Watanzania bila kujali tofauti za kiitikadi, kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika zoezi hilo muhimu.

Amesema kuwa ni haki ya msingi kwa kila raia kujiandikisha na kushiriki katika uchaguzi.

Aidha, ameeleza furaha yake kwa kutimiza jukumu hilo muhimu la uraia na kuonyesha kuridhishwa na utaratibu mzuri uliowekwa kwa ajili ya zoezi hilo.