Serikali yaanza majaribio ya GMO

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 07:07 PM Oct 16 2024
Mbegu za GMO.
Picha:Mtandao
Mbegu za GMO.

SERIKALI imetangaza rasmi kuanza kuvitumia Vituo vya Utafiti vya Mikocheni cha Jijini Dar es Salaam na Makutupora cha Jijini Dodoma kwaajili ya kufanya majaribio na utafiti wa mbegu zenye vinasaba vya uhandisi jeni maarufu kama GMO.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema hayo leo Oktoba 16,2024 wakati akizungumza na wanajumuiya wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA. 

Wanajumuiya hao ni wanataaluma, wadau waliowahi kusoma na kufanya kazi katika  chuo hicho katika halfa iliyotanguliwa awali na utoaji wa zawadi kwa wanafunzi na wahadhiri waliofanya vizuri kitaaluma.

 Waziri Bashe amesema serikali wameridhia uamuzi huo licha ya kwanza teknolojia hiyo haijaruhusiwa rasmi matumizi yake nchini kwa lengo la kujiweka tayari kwa kuwa na wataalamu watakaokuwa tayari wakati wowote.

 Amesema maabara maalum za kiuchunguzi zitajengwa na majaribio yatafanyika. "Hata kama nchi haijaruhusu sasa, hatuwezi kuwa kama kisiwa kwamba hatujui kinachoendelea, Kenya hapo wameshaanza kuzitumia, na hata kwa mikoa ya mipakani hazishindwi kuingia wakati wowote, hata kama mipakani tumezidi kuimarisha udhibiti wa uingiaji wa mbegu na kuweka masharti magumu,"alisema Waziri Bashe.

 Aidha, amesema pia serikali iko kwenye mchakato wa maboresho ya mifumo na ya kikanuni kwenye sekta ya kilimo, ili kuzitambua na kuruhusu rasmi matumizi ya mbegu za asili nchini.

 Kuhusu wataalam wa ugani, Waziri huyo wa Kilimo alithibitisha kuwa  bado kuna changamoto kubwa ya wagani ambapo kuna changamoto ya upungufu wa maafisa ugani kwa zaidi ya asilimia 67.

 Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo SUA, Prof. Raphael Chibunda akaiomba serikali kuiingiza SUA kama eneo la tatu la majaribio ya GMO kutokana na uwezo mkubwa walio nao hasa kwenye utaalamu, vifaa na watafiti.

 "Muda mrefu tulishindwa kufanya utafiti kwenye eneo hili kutokana na vikwazo kwasababu utafiti wowote lazima pia uwe na majaribio, lazima ufike shambani na kuona matokeo, tulishindwa kuanzisha maabara ya utafiti wa GMO kwa kushirikiana na watafiti kutoka nje walioonesha nia kwa kufungwa na kanuni mbalimbali zilizoonekana tishio kwa watafiti,"amesema Prof Chibunda