Wakulima wa tumbaku Tabora waiomba serikali kuwasaidia kupata pesa zao

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 07:37 PM Oct 16 2024
Mwenyekiti wa chama hicho, Umuiya Musoma.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa chama hicho, Umuiya Musoma.

WAKULIMA 61 wa tumbaku wa Chama cha Msingi Itegamatwi kilichopo Kitongoji cha Uyela, Kata ya Usoke Wilaya ya Urambo mkoani Tabora wameiomba serikali kuwasaidia kusimamia mchakato wa kupata pesa zilizositishwa na Benki ya Azania ili waweze kurudi shambani.

Awali walishaahidiwa kupata pembejeo kutoka benki hiyo ambapo walishakamilisha hatua za awali za kuandaa mashamba kujitayarisha na kilimo hicho.

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa chama hicho, Umuiya Musoma amesema wamesikitishwa na kitendo cha kusitishwa kwa upataji wa pembejeo uliokuwa na makisio ya dola za kimarekani 87,254.76  ili waweze kuendelea na kilimo hicho kwa msimu huu.

Amesema awali makisio hayo yalishakubaliwa na kupitishwa na Mrajisi Msaidizi wa Mkoa Tabora Juni 15, 2024 na benki kupitisha kwa taratibu zilizowekwa lakini ilipofika Septemba 13, 2024 walikuja kujibiwa kuwa hawataweza kupatiwa fedha hizo.

Amesema jambo hilo limewasikitisha kwa kuwa walitegemea kupata fungu hilo kwa asilimia zote kwakuwa benki hiyo ndio inawahudumia kwakila msimu hali iliyowafanya wakulima kushindwa kuendelea na kilimo kutokana na mkwamo huo.  

Amesema kitendo cha awali kuahidiwa kupatiwa pembejeo hizo tayari walishaanza kuandaa mashamba na kuwa na utayari wa kuanza kwa msimu mwingine wa kilimo lakini baadae walivyoambiwa hawawezi kupatiwa vitahudumiwa  vyama ambavyo havikufanya vizuri kwa msimu uliopita.

“Tumechanganyikiwa maana tumeajiri wafanyakazi mashambani na wameshafanya maandalizi ya kilimo, kuna watu wasipolima tumbaku hawawezi kuishi, watoto wao hawaendi shule’

“Nimechukua uamuzi wa kuja huku Dar es Salaam niongee na vyombo vya habari mimi kama Mwenyekiti niliyobeba maono ya wengine ili kilio chetu kimfikie Waziri mwenye dhamana Hussen Bashe  na Rais Samia Suluhu aweze kutusaidia tupewe pembejeo ili turudi shambani ”amesema

Amefafanua zao la tumbaku kama litasimamiwa vyema na serikali basi wakulima hasa waishio vijijini litaweza kuwakomboa kwani linaleta tija kwa wakulima kwani zao hili ni la kimkakati linalimwa kwa msimu.