Stars bado haijakata tamaa, kocha akisema viwango vimeamua mechi

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:52 PM Oct 16 2024
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco.
Picha: Azam TV
KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco.

KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman 'Morocco', amesema licha ya kupoteza mabao 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, lakini bado hajakata tamaa ya kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, (AFCON), akiwasihi pia Watanzania wasivunjike moyo kwani kufungwa siyo mwisho wa safari.

Akizungumza jana baada ya mchezo wa Kundi H, kusaka tiketi ya kucheza AFCON mwakani nchini Morocco, kocha huyo alisema kupoteza mchezo huo wa jana kulichangiwa zaidi na viwango vya mchezaji mmoja mmoja kwa timu zote mbili.

Alisema pamoja na wachezaji wa Tanzania kujitahidi na kutoa jasho lao lote uwanjani, lakini walihukumiwa na ukosefu wa umakini dakika za mwisho za mchezo.

"Tumepoteza mechi, kwa mimi naona viwango vimeamua mechi. Viwango vya mcchezaji mmoja mmoja vimefanya matokeo kuwa kama yalivyokuwa.

Ukiangalia katika mchezo huu tumecheza vizuri, hasa kipindi cha kwanza tumejaribu kutengeneza nafasi, bahati mbaya hatukuweza kuzitumia, wenzetu walivyorejea kipindi cha kwanza walijaribu kusukuma mashambulizi mengi kwetu, tulilazimika kuumiliki mpira kadri muda ulivyozidi kwenda, lakini dakika za mwisho ukosefu wa umakini, umesababisha tumepoteza mechi," alisema kocha huyo.