Mapya yaibuka mbele ya seneti, kesi ya Naibu Rais Kenya

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 08:16 PM Oct 16 2024
Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Picha: Mtandao
Naibu Rais Rigathi Gachagua.

GAVANA wa Kaunti ya Siaya nchini Kenya, Wakili Mwandamizi James Orengo ametetea msukumo wa kumwondoa Naibu Rais Rigathi Gachagua ofisini akimshutumu kwa kupata pesa kwa njia isiyo ya kawaida kutoka kwa akaunti za marehemu kaka yake, Nderitu Gachagua.

Orengo ameeleza hayo leo Oktoba 16, 2024 mbele ya Seneti akibainisha mashaka yake kuhusu jinsi Gachagua alivyotekeleza wosia wa kaka yake ambao umekuwa mada ya kesi ya kumng'oa mamlakani.

Alidai kuwa Naibu Rais ‘aliivamia’ akaunti za kaka yake na kutumia mapato hayo kupata mali kuu ikiwa ni pamoja na hoteli za kifahari za Treetops na Outspan katika Kaunti ya Nyeri.

Wakati Gachagua akishikilia kuwa sehemu kubwa ya utajiri wake ulitokana na urithi wake kutoka kwa kaka yake, Orengo, anayewakilisha Bunge la Kitaifa katika kesi ya kumuondoa madarakani, alihoji kuwa utekelezaji wa wosia huo unaibua mashaka.

Orengo alidokeza kuwa Gachagua alianza kutoa pesa kutoka kwenye akaunti za marehemu Nderitu siku ambayo gavana huyo alifariki dunia.

Ameendelea kudai kuwa Gachagua alisafiri kwenda London, ambako kaka yake alikuwa akipokea matibabu maalum, Februari 16, 2017. Siku iliyofuata, alidaiwa kumfanya kaka yake asaini wosia. Alidai wiki moja baadaye, yaani Februari 24, 2017, Nderitu Gachagua alipoaga dunia, Orengo anadai Gachagua alikuwa tayari ameanza kutoa pesa kutoka kwa akaunti za marehemu kaka yake.

Orengo amemshutumu Gachagua kwa kupata mali za ziada kupitia fedha alizopata kwa njia isiyo ya kawaida kutoka kwa kaka yake marehemu.

"Alikwenda hospitali mjini London ambako kaka yake alilazwa ICU. Alipofika siku iliyofuata, alimshawishi ndugu yake kutekeleza wosia... Hiyo ilikuwa Februari 17, 2017. Hakuna ushahidi kwamba alizungumza na madaktari waliokuwa wakimuhudumia huyo ndugu yake na baada ya hatua hiyo, aliondoka..." Orengo alidai mbele ya Seneti.

Aliendelea, kudai kuwa jinsi akaunti za ndugu yake zilivyopatikana ziliendelea hadi upatikanaji wa Bustani za Mizeituni kupitia wakala. Pia alinunua mali katika Nyeri, ikiwa ni pamoja na hoteli za Outspan na Treetops.

"Ushahidi utaonyesha kwamba alikuwa akivamia fedha ambazo kwa kweli zilikuwa mali ya kaka yake marehemu ili kupata mali. Kama hilo si kosa, kwa mujibu wa sheria. Haya ni mapato ya uhalifu uliofanywa na Naibu Rais kupata mali... Tunasema, kupatikana kwa mali hizi kulitokana na mwenendo wa uhalifu," alihitimisha Orengo.

Wakili Elisha Ongoya, ambaye anawakilisha Naibu Rais Gachagua katika kesi hiyo, alipuuzilia mbali madai ya Orengo na kulita kuwa ni kama jaribio la kuchochea hisia za umma dhidi ya Naibu huyo wa Rais.

Shauri hilo limetua mapema leo mbele ya seneti na kuanza kusikilizwa majira ya saa nne asubuhi ambako Naibu Rais Gachagua aliwasili Seneti ambako kulionekana kuwa na ulinzi mkali wa askari wa taifa hilo sambamba na walinzi wa usalama wa Gachagua.