Sababu mbili zapaisha nauli za boti Dar-Z'bar

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:36 AM Oct 16 2024
Sababu mbili zapaisha nauli za boti Dar-Z'bar
Picha:Mtandao
Sababu mbili zapaisha nauli za boti Dar-Z'bar

NAULI za usafiri wa majini Dar es Salaam-Zanzibar zimepanda. Wananchi wanalalama ugumu wa maisha umeongezeka.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar, Mtumwa Said amesema kuongezeka kwa bei ya mafuta ya meli kumesababisha kupanda kwa bei ya nauli ya boti kutoka Sh. 30,000 ya awali hadi Sh. 35,000 sawa na ongezeko la Sh. 5,000 (asilimia 16.7).

Mtumwa alisema jana visiwani Zanzibar kuwa ongezeko hilo la bei ya mafuta limesababisha gharama za uendeshaji kuongezeka kwa asilimia 21.

Mkurugenzi Mtumwa alisema kupanda kwa bei ya dola sokoni kumechangia ongezeko la nauli kwa kuwa kampuni za usafirishaji majini (boti) zinapolipa kodi, kununua vifaa na kufanya matengenezo ya vyombo vyao, hulipa kwa dola.

Alisema kuwa mwaka 2022, dola ya Marekani iliuzwa kwa wastani wa Sh. 2,330, lakini mwaka huu, inauzwa kwa wastani wa Sh. 2,850 katika soko la kawaida, hivyo kufanya kuwapo ongezeko la gharama za uendeshaji.

Mkurugenzi huyo alisema serikali imeridhia kampuni za uwekezaji zinazotoa huduma za usafiri wa baharini kuongeza bei za nauli za usafiri kati ya Dar es Salaam na Unguja kwa daraja la chini kutoka Sh. 30,000 hadi 35,000. Nauli mpya zilianza kutumika rasmi Oktoba 7, mwaka huu.

Alifafanua kuwa nauli ya Sh. 30,000 kwa daraja la chini ilitangazwa mwaka 2022, kipindi ambacho bei ya mafuta ilikuwa Sh. 2,500 kwa lita kulinganishwa na mwaka huu ambapo bei ya mafuta ni Sh. 3,020.

Sababu nyingine, Mtumwa alisema ni gharama za matengenezo na utawala, kampuni zikilalamika kuongezeka gharama za utawala na matengenezo ya vyombo kipindi hiki ambacho dola imepanda.

"Bei iliyopendekezwa awali ilikuwa zaidi ya Sh. 35,000 iliyokubaliwa. Serikali kwa kuzingatia hali za maisha ya wananchi wake, hasa wa daraja la chini, katika mazungumzo yaliyofanyika, tuliwaomba sana wawekezaji, kampuni hizi kukubali ombi la serikali kufikia Sh. 35,000 kwa daraja la chini na kampuni zilitukubalia," alisema.

Mtumwa aliwataka wadau wote wa usafirishaji baharini kuzingatia bei iliyoidhinishwa na serikali. Atakayekiuka, atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Hata hivyo, nauli ya boti kutoka Unguja kwenda Pemba haijapanda, imeendelea kuwa Sh. 20,000 kwa daraja la chini.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Nipashe jana, walisema nauli mpya zitaongeza ukali wa maisha, wakiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuweka ruzuku ili kuwasaidia wananchi wa kipato duni.

Said Ali Abdalla, Salma Juma Khalfan na Rahma Abadalla Mussa, wakiwa eneo la kukata tiketi za boti, jijini Dar es Saalam jana, walisema wamesikitishwa na ongezeko hilo la nauli kwa kuwa wananchi wengi hali zao ni duni.

Mwajuma Ally aliomba serikali iwasaidie wananchi nauli ishuke iwe kama ilivyokuwa awali, akisema: "Kupanda kwa nauli kunatuumiza kibiashara, ongezeko la Sh. 5,000 kwa wafanyabiashara wadogo linakata faida yetu."

Msafiri mwingine Yona Mwenda aliyekuwa amewasili Dar es Salaam akitokea Zanzibar, alisema, "Mtu umejiandaa nauli ya Sh. 30,000 unafika feli unaambiwa nauli imepanda kwa 5,000, maana yake inatakiwa kulipia Sh. 35,000. Hii si sawa, uwekwe utaratibu mzuri wa kudhibiti bei kupanda kiholela," alisema Mwenda.

*Imeandikwa na Rahma Suleiman (ZANZIBAR) na Halfani Chusi (DAR)