Wakili alalama kesi ya 'afande' kuendelea bila mhusika kuwapo

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 01:01 PM Oct 16 2024
Mahamaka ya Wilaya ya Dodoma.
Picha: Mtandao
Mahamaka ya Wilaya ya Dodoma.

MAHAKAMA ya Wilaya ya Dodoma leo inatarajiwa kuanza kusikiliza shauri linalomkabili Fatma Kigondo, maarufu Afande, anayeshtakiwa kwa madai ya kuwatuma vijana kumbaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Saalam.

Kogondo anakabiliwa na shtaka la kubaka kwa kundi kinyume cha kifungu cha sheria namba 131 A kifungu kidogo cha pili ambacho kinasema anayewasaidia wahalifu kutenda kosa la ubakaji na yeye anahusika kwenye ubakaji wa kundi. 

Hakimu Mkazi Mwandamizi, Nyamburi Tungaraja, alisema mahakamani hapo jana kuwa shauri hilo litaanza kusikilizwa leo bila kujali kama mshtakiwa atakuwapo au la. 

“Shauri hili litaanza kusikilizwa kesho (leo) bila kujali kama mshtakiwa atakuwapo au hatakuwapo. Kwa hiyo tukutane kesho saa 3:00 asubuhi,” alisema Hakimu Tungaraja. 

Kuhusu maombi ya wakili wa mlalamikaji, Peter Madeleka, ya kukamatwa na kuwekwa rumande mshtakiwa kwa sababu za usalama wake, Tungaraja alisema hawezi kutoa amri ya kumkamata mtu kwa kushindwa kufika mahakamani mara moja. 

“Siwezi kutoa amri ya kukamatwa kwa mshatakiwa kwa kushindwa kuja mara moja mahakamani. Lakini pia ugonjwa ni sababu ambayo ipo kisheria, hivyo kesi hii itaendelea tu hata kama hatakuwapo ama atakuwapo kesho (leo) mahakamani lakini pia dhamana ni haki ya mshtakiwa,” alisema. 

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama, Wakili Madeleka alisema hawakubaliani na mwenendo wa shauri hilo linavyoendeshwa na hakimu huyo na wanajiandaa kulihamishia mahakama kuu. 

“Mshtakiwa siku ya kwanza hakuja na leo (jana) pia hajafika lakini leo (jana)  ilikuwa siku ambayo mahakama hii inakwenda kutoa uamuzi kuhusu maombi yangu mawili, likiwamo la kukamatwa na kuwekwa rumande kwa mshtakiwa  kwa sababu za kiusalama kama ilivyo kuwa kwa watuhumiwa wengine kina Nyundo na wenzake. Pia ombi la pili lilikuwa mahakama kutoa adhabu kwa mshtakiwa ya kukiuka amri ya mahakama na kushindwa kufika wakati wa shauri. 

“Lakini tunashangaa leo hii hakimu anasema yeye hawezi kutoa amri ya mahakama kukamatwa na kuwekwa rumande kwa mtuhumiwa huyo kwa madai kuwa dhamana ni haki ya mshtakiwa kwani wale kina Nyundo walikuwa hawana haki ya dhamana. Tunafahamu kuwa makosa kama haya ya ulawiti mahakama huwa inaondoa dhamana kwa washtakiwa na kuwaweka rumande kwa sababu za kiusalama,” alisisitiza Madeleka.

Shauri hilo ambalo lilipangwa kusikilizwa Oktoba 7, 2024 liliahirishwa hadi jana baada ya mshtakiwa kutofika mahakamani kwa madai kuwa ni mgonjwa. Siku hiyo  Wakili Madeleka aliiomba mahakama kutoa amri ya kukamatwa kwa Kigondo na kumwekwa rumande katika Gereza la Isanga jijini hapa. 

Wakili Madeleka alisema anaiomba mahakama hiyo kutoa amri hiyo ili mshtakiwa huyo akamatwe mara moja na kunyimwa dhamana kama ilivyokuwa kwa washtakiwa wengine.

"Mheshimiwa hakimu tunaomba mahakama yako tukufu itoe amri ya mshtakiwa kukamatwa na kuwekwa rumande na kuondolewa dhamana kwa sababu ya usalama wake kama ambavyo mahakama imekuwa ikitoa amri hizi kwa washtakiwa wengine. 

“Lakini pia kutokana na mshtakiwa kutofika mahakamani hapa amevunja amri ya mahakama ambayo inamtaka kufika kila tarehe ya shauri lake, hivyo tunaomba mahakama itoe adhabu kali mara moja kwa mshtakiwa kuvunja amri ya mahakama ya kumtaka kufika kila shauri linapoendeshwa kwani kukosekana kwake hapa leo kesi hii haiwezi kuendelea,” alisema Madeleka. 

“Kama anaumwa lazima wangeleta ushahidi wa daktari kama ambavyo wanatakiwa kufanya kwa mujibu wa sheria lakini hii kusema tuu mtu anaumwa siyo kazi ya mahakama kubaini kama mtu anaumwa kweli au haumwi walipaswa kuleta ushahidi wa kimatibabu hapa siyo kuzungumza tu,” alihoji wakili Madeleka.

Hakimu Tungaraja aliahirisha shauri hilo hadi leo na hoja hizo zinatarajiwa kutolewa uamuzi.