Wakulima wafurahia kupanda bei ya korosho

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:05 PM Oct 16 2024
Korosho.
Picha: Mtandao
Korosho.

WAKULIMA wa korosho Wilaya ya Masasi, Mtwara na Nanyumbu wa Chama Kikuu cha Ushirika (MAMCU) wamejikuta wakibubujika na machozi ya furaha baada ya kuuza korosho zaidi ya tani 18, 000 kwa bei ya juu ya Sh. 4,195 na bei ya chini Sh. 3,440.

Imedaiwa kuwa bei hizo hazijawahi kutokea miaka 10 iliyopita katika minada ya zao la korosho kwa mikoa ya Kusini.

Mnada wa kwanza wa korosho msimu wa 2024/2025 wa chama hicho uliofanyika katika kijiji cha Nakachindu, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, tani zaidi ya 18,000 za korosho ziliuzwa kwa njia ya mfumo wa soko la bidhaa (TMX).

Wakizungumza katika mnada huo baadhi ya wakulima walisema kuwa bei hizo hazijawahi kutokea katika misimu ya hivi karibuni kwenye zao la korosho.

Feith Milanzi, mkulima wa kijiji cha Nakachindu alisema kuwa bei ya Sh. 4,195 kwa bei ya juu na Sh.3,440 bei ya chini zinaleta matarajio makubwa katika maisha yao.

Alisema matunda hayo ya bei nzuri katika mazao ya biashara hasa korosho yanatokana na uongozi bora wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Naye Faraja Hassani, mkulima kutoka wilaya ya Nanyumbu alisema takribani miaka saba hadi kumi iliyopita bei ya zao la korosho ilikuwa chini na kuwakatisha tamaa wakulima kulima zao hilo.

"Tunampongeza Rais Dk. Samia Suluhu kwa kusikiliza kilio chetu wakulima cha kutaka bei za mazao hasa korosho kuwa bora kwa wakulima na leo tunaona bei zimekuwa juu sana na kila mkulima ameridhika," alisema. 

Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred, alisema bei za mazao zitaendelea kuwa nzuri na wakulima watafaidika.

Alisema Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na serikali imesimamia bei ya mazao hasa zao la korosho kuhakikisha inakuwa bora zaidi.

Biadia Matipa, Meneja wa Chama Kikuu Cha Ushirika (MAMCU), alisema katika msimu huu wa korosho mwaka 2024/2025 bei ya korosho itaendelea kuwa nzuri.

Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Loutery Kanoni aliwataka wakulima watakapopata fedha kutumia vizuri ikiwamo kupeleka watoto shuleni na kuacha kuzitumia katika sherehe za vigodoro ambazo hazina msingi kwao.