DC Magoti aahidi kuendeleza miundombinu ya unawaji mikono

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 04:47 PM Oct 16 2024
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Peter Magoti.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Peter Magoti.

MKUU wa Wilaya ya Kisarawe, Peter Magoti, ameahidi kuendeleza na kutunza miundombinu ya unawaji mikono iliyojengwa na Shirika la WaterAid katika uhamasishaji wa watu kunawa mikono.

Magoti aliyasema hayo katika maadhimisho ya siku ya kunawa mikono iliyofanyika katika Shule ya Msingi Kazumzumbwi wilayani ya Kisarawe ambapo siku hii huadhimishwa  ifikapo Oktoba 15, duniani kote.

Magoti amesema katika kampeni hiyo, Shirika hilo limewafanyia mambo mengi ikiwemo ujemzi wa miundombinu ya vyoo na kunawa mikono katika shule 30 na vituo 15 vya afya hivyo hawana budi kuvitunza ili viwasaidie  kulinda afya za wanamchi na wanafunzi. 

Aidha, amesema siku ya kunawa mikono ni muhimu katika kutoa elimu kwa jamii ukizingatia mkono ndio kila kiti na itawaepusha na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya tumbo, macho, kichocho, kipindupindu, kuhara na magonjwa ya homa ya tumbo.

Naye Kaimu Mkurugezi wa Shirika la WaterAid, Christina Mhando, amesema lengo kuu la mradi wa unawaji mikono  ni kuhamasisha tabia siha kwa wananfunzi, watoa huduma za afya, walimu na jamii kwa ujumla.

Amesema huwa wanatumia siku hiyo kuwashawishi watunga sera watoa maamuzi, wafadhili na wadau mbalimbali umuhimu wa kuwekeza kwenye maji na usafi wa vyoo na kunawa.

"Tunatoa wito kwa jamii kuona umuhimu wa kunawa mikono kwa jamii kujikinga na magonjwa na kwa watoa huduma kuwakinga wale wanaowahudumia,"amesema.

Naye Junita Maiko mwanafunzi  wa shule ya Msingi Sungwi amesema katika maadhimisho hayo amejifunza mambo mbalimbali kubwa umuhimu wa unawaji mikono huku akiahidi kwenda kuwa balozi mzuri kwa jamii inayomzunguka.

Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Sungwi, Shabani Dude, alisema mradi huo umewasaidia hususani katika kuwajengea miundombinu na kulinda afya za wanafunzi.