Adaiwa kumuua mtalaka wake, naye ajaribu kujiua kwa kujichoma kisu

By Moses Ng’wat , Nipashe
Published at 05:58 PM Oct 16 2024
Silaha ya jadi iliyotumika kukatisha uhai
Picha: Mtandao
Silaha ya jadi iliyotumika kukatisha uhai

MKAZI wa Kijiji cha Kapeta, Kata ya Ikinga, wilayani Ileje, mkoani Songwe, Wema Ndile (29) ameuawa kwa kuchomwa na kisu kwenye kitovu na shingoni na mtalaka wake waliyetengana miezi mitano iliyopita.

Aidha, mtuhumiwa huyo, Ally Mwakilembe (42) alijaribu kujiua kwa kujichoma kwa kisu tumboni baada ya kutekeleza mauaji hayo, na sasa amelazwa katika moja ya hospitali wilayani humo.

Taarifa zilizopatikana kutoka eneo la tukio zilizothibitishwa na Mtendaji wa Kijiji cha Kapeta, Octatus Wangu, zinaeleza kuwa mwanaume huyo alitekeleza mauaji ya mtalaka wake huyo baada ya kumvamia usiku wakati amelala katika chumba alichokuwa amepanga. 

Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hii, Mtendaji wa Kijiji cha Kapeta, Wangu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea majira ya saa nane usiku ya Oktoba 16, 2024.

Amesema kuwa kabla ya mauaji hayo kutokea, mtuhumiwa alikuwa katika harakati za kumshawishi mtalaka wake warudiane baada ya kutengana kwa miezi mitano.

Amesema kuwa ndoa ya wawili hao ilidumu kwa kipindi cha miaka 10 na kufanikiwa kupata watoto wawili, lakini baadaye mwanamke (marehemu) aliamua kutengana na mumewe kwa kile alichoeleza watu kuwa alikuwa mlevi kupita kiasi na kushindwa kutekeleza majukumu ya familia.

Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida gari la wagonjwa lilinusurika kuchomwa moto na wananchi wenye  hasira kali wakipinga kitendo  cha kutaka kumuwahisha majeruhi hospitali wakitaka naye afie hapo.

Kutokana na hali hiyo majeruhi huyo kukaa zaidi ya saa 10, huku utumbo wake ukiwa nje akisubiri msaada wa jeshi la polisi wa Kituo Kikuu cha Wilaya ya Ileje, kilichopo umbali wa zaidi ya 100 ambapo baada ya kufika eneo la tukio walilazimika kuwatanya wananchi hao wenye hasira na kisha kumchukua majeruhi huyo.

Jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Agostino Senga hazikufanikiwa kwa kile kilichoelezwa kuwa yuko nje ya ofisi na hata simu zake hazikupatikana.