Wakili Madeleka ataka ‘Afande’ kusomewa mashtaka hospitalini

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 11:30 AM Oct 17 2024
Wakili Peter Madeleka.
Picha: Mtandao
Wakili Peter Madeleka.

SAKATA la kesi inayomkabili Fatma Kigondo, maarufu Afande, jana lilichukua sura mpya baada ya wakili wa upande wa mlalamikaji, Peter Madeleka, kuomba Mahakama ya Wilaya ya Dodoma kumsomea mashtaka katika hospitali aliyolazwa ili hatua zingine za kisheria ziendelee.

Kigondo anakabiliwa na shtaka la kubaka kwa kundi kinyume cha kifungu cha sheria namba 131 A kifungu kidogo cha pili ambacho kinasema anayewasaidia wahalifu kutenda kosa la ubakaji na yeye anahusika kwenye ubakaji wa kundi.  

Mshtakiwa huyo ambaye alipaswa kufika mahakamani Oktoba 7, mwaka huu, kusikiliza shtaka linalomkabili, hakufanya hivyo kwa madai yaliyotolewa na wakili wake Sedrick Mbunda kuwa ni mgonjwa. 

 Baada ya kauli hiyo Wakili Madeleka, alitoa maombi hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, Nyambuli Tungaraja. 

Katika maombi yake, Wakili Madeleka, aliiomba mahakama hiyo kutia saini malalamiko yaliyowasilishwa na mlalamikaji Paul Kisabo, mahakamani hapo dhidi ya Kigondo ili yatumike kama hati ya mashtaka. 

“Mweshimiwa Hakimu tunaiomba mahakama yako tukufu kusaini malalamiko haya tuliyowasilisha dhidi ya Fatma Kigondo ili yatumike kama hati ya mashtaka na baada ya kusainiwa mshtakiwe asomewe mashtaka yake katika hospitali yoyote alipo bila kujali anaumwa ugonjwa gani. Iwe Muhimbili, Benjamini Mkapa, Bugando au sehemu yoyote ili hatua zingine za kisheria ziendele,” alidai Madeleka. 

Baada ya maombi ya wakili huyo, Hakimu Tungaraja aliahirisha kesi hiyo hadi kesho atakapotoa uamuzi baada ya kupitia baadhi ya mifungu vya sheria. 

Aidha, akizungumza nje ya mahakama, Wakili Madeleka alisema jana walipanga kupeleka maombi yao ya marejeo Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma ili ikaangalie mwenendo wa shauri hilo hadi sasa kwa sababu kumekuwa na hila na fitina nyingi. 

“Mara hakimu aliyekuwapo kahamishwa mara wanasema hakimu hajapangiwa, mara hakimu aliyepangiwa anasema mahakama si kazi yake kwenda kumkamata mshtakiwa kwamba dhamana ni haki ya mshtakiwa, yaani vitu ambavyo havieleweki. 

“Mahakama inakuwa inajichanganya sasa tunaona badala ya kupoteza muda na rasilimali fedha tunakuwa tunakuja hapa kwa vitu visivyoeleweka ni bora twende kwa watu wanaojielewa wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma,” alisema. 

Alisema Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma itafanya mapitio kwenye kesi hiyo ili kuona mwenendo wa kesi hiyo kama unakwenda kwa mujibu wa sheria ama vinginevyo na ikioneka mahakama inakiuka sheria Mahakama Kuu inayo mamlaka ya kutoa maelekezo nini kifanyike ili haki iweze kutendeka kwa pande zote mbili,” alisisitiza.