Samia aikabidhi tuzo NSSF usimamizi, uratibu hifadhi ya jamii sekta binafsi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:05 PM Oct 17 2024
Samia aikabidhi tuzo NSSF usimamizi, uratibu hifadhi ya jamii sekta binafsi
Picha: Mpigapicha Wetu
Samia aikabidhi tuzo NSSF usimamizi, uratibu hifadhi ya jamii sekta binafsi

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeshinda tuzo ya Usimamizi na Uratibu wa Hifadhi ya Jamii kwa Sekta Binafsi nchini, wakati wa kilele cha Maonesho ya Saba ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika kwenye uwanja wa EPZ Bombambili, mkoani Geita.

Tuzo hiyo imetolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na kupokewa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, wakati wa ufungaji wa maonesho hayo.

Aidha, NSSF imeshinda tuzo ya mshindi wa kwanza katika kundi la Hifadhi ya Jamii na Huduma za Bima zilizotolewa Oktoba 12, 2024 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, wakati wa maonesho hayo.

Mshomba alisema utoaji wa huduma kidijitali umekuwa nyenzo muhimu katika kuhakikisha huduma za NSSF zinawafikia wanachama popote walipo, ikiwamo kufungua madai ya kuomba mafao mbalimbali.

Aliwataka waajiri wa sekta binafsi kusajili wafanyakazi wao NSSF pamoja na kuwasilisha michango kwa wakati, kwa kuwa hilo ni takwa la sheria na vilevile kuwezesha Mfuko kuendelea kukua na kutoa huduma bora.

Aidha, Mshomba alitoa rai kwa watu waliojiajiri katika sekta isiyo rasmi wakiwamo wachimbaji wadogo wa madini, mamalishe, babalishe, bodaboda, wavuvi, wakulima, wafugaji na wajasiriamali mbalimbali kujiunga na kuchangia NSSF kwa sababu ndiyo njia sahihi ya kupunguza umasikini wa kipato na kujikinga dhidi ya majanga mbalimbali.

Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji, Omary Mziya, amesema mfuko utaendelea kutoa huduma bora kwa wanachama kupitia mifumo ya TEHAMA na hivi sasa wanachama wanaweza kufungua madai yao kwa njia ya kidijitali bila ya kulazimika kufika katika ofisi za NSSF.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa NSSF, Lulu Mengele, alisema kupitia maonesho hayo Mfuko ulifikisha elimu ya hifadhi ya jamii kwa makundi mbalimbali yakiwamo ya wachimbaji wadogo wa madini pamoja na wajasiriamali zaidi ya 1,500 wilayani Bukombe. "Maonesho ya madini yalikuwa fursa kwa NSSF kufikisha elimu ya hifadhi ya jamii, kuandikisha wanachama wapya kutoka sekta isiyo rasmi, tutoe elimu kuhusu huduma za kidijitali pamoja na fursa za nyumba na viwanja," alisema Lulu.

Awali, Meneja wa NSSF Mkoa wa Geita, Winniel Lusingu alisema katika mwaka wa fedha 2024/25, Ofisi ya Mkoa huo imeweka lengo la kukusanya Sh. bilioni 104 na kuwa mwaka wa fedha uliomalizika walikusanya Sh. bilioni 64. Alishukuru ushirikiano mkubwa wanaopata kutoka kwa uongozi wa mkoa huo, waajiri, menejimenti na wafanyakazi wote wa NSSF.