Biteko: Serikali imetoa ruzuku mitungi 400,000

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 11:42 AM Oct 17 2024
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.
Picha:Mtandao
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko.

SERIKALI imetoa ruzuku kwa mitungi zaidi ya 400,000 ya gesi ya kupikia (LPG), ambayo itaanza kugawiwa kwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini mwishoni mwa mwaka huu.

Lengo la kufanya hivyo ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo kwa sasa inapigiwa chapuo, ili kulinda afya za wananchi na kutunza mazingira.

 Ikumbukwe kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yanaokoa muda, unatumika muda wa saa mbili kwa wiki kupika, huku nishati chafu kama vile kuni na mkaa ikitumia saa saba kwa wiki.

 Katika Kongamano la Tisa la Nishati na Biashara Afrika, lililofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili, lijadili namna nchi hizo zitakavyokuwa na nishati ya uhakika ya umeme.

 Akifungua kongamano hilo, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, alisema ugawaji wa mitungi ya gesi yenye ruzuku ni hatua ya serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati ya kupikia.

 Kuhusu sababu ya kwa kuelekeza nguvu ya kutumia nishati ya gesi LPG  kuliko nyingine, alisema mkakati wa serikali kuhamasisha matumizi ya nishati ya kupikia  unahusisha vyanzo vyote  vikiwamo vya umeme jua na mkaa mbadala na wanaendelea kuweka mazingira rafiki ili kutumika.

 “Serikali inahamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwamo inayotokana na umeme jua, mkaa mbadala na gesi ambavyo tumetoa ruzuku na wananchi watapata mitungi kwa bei nafuu, kuhusu usalama wa gesi nakiri haina madhara na hadi sasa hakuna visa vyovyote vilivyoripotiwa tangu tuanze kuhamasisha matumizi yake,” alisema Dk. Biteko.

 Tanzania imekuwa nchi kinara katika uhamasishaji wa matumizi ya nishati mbadala, pia imefanikiwa kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme kwenye maeneo mbalimbali.

 Dk. Biteko alisema hadi kufikia mwezi Desemba, mwaka huu, vijiji 12,000 vitaunganishwa na huduma ya umeme kupitia Wakala wa Huduma za Nishati Vijijini (REA).

 Aidha, Tanzania ina mchango wa kuhakikisha watu milioni 300 katika Bara la Afrika wataunganishwa na huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.

 Alisema mapema mwezi Januari 2025, Tanzania itaandaa mkutano wa kujadili masuala ya nishati safi na upatikanaji wa umeme kwenye nchi za Afrika na miongoni mwa majadiliano ni pamoja na kupata namna ya kufanikisha kuwaunganishia nishati ya umeme watu milioni 300  kwenye nchi zote.

 “Tumepata heshima kuandaa mkutano mkuu wa nchi za Afrika kujadili masuala ya nishati safi ya kupikia na umeme, ni baada ya kuona tumefanya vizuri katika kutekeleza miradi mbalimbali ambayo mingine imekamilika na kubakia na akiba ya umeme ambao tunaweza kuuza kwenye mataifa mengine,” alisema Biteko.

 Msimamizi wa Mkutano huo, Dk. Patricia Laverley ambaye ni Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), alisema wanaungana na serikali kutekeleza miradi mbalimbali inayohusu matumizi ya nishati safi ya kupikia. 

Aidha, alisema wanafanya hivyo ili kumwezesha mwanamke kutumia nishati safi kulinda afya yake na kuokoa muda ambao mara nyingi anautumia kutafuta nishati isiyo rafiki wa mazingira.

 Mwenyekiti wa Nishati, Mabadiliko ya Tabianchi na Uchumi wa Kijani kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk. Kevin Kariuki, alisema watashirikiana na wadau wengine kupiga debe jitihada zinazofanywa na serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia. 

Rais Samia Suluhu Hassan ameibeba ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia Barani Afrika, huku Tanzania ikiweka malengo ya kufikia asilimia 80 ya Watanzania ifikapo 2030.
Mwisho