Uchumi rejeshi kuboresha maji kwenye Ziwa Tanganyika

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 03:44 PM Oct 17 2024
Uchumi rejeshi kuboresha maji kwenye Ziwa Tanganyika.

TAASISI ya Catholic Relief Services (CRS) kwa kushirikiana na Taasisi Caritas wameanzisha mradi wa uchumi rejeshi katika maeneo yanayozunguka Ziwa Tanganyika, ili kuongeza ubora wa maji katika ziwa hilo na kuinua uchumi wa wananchi.

Mradi huo unalenga kuongeza uelewa wa namna ya kubadilisha taka kuwa fursa na kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya teka rejeshi kwa makundi mbalimbali kuanzia ngazi ya jamii,wafanyabiashara taasisi binafsi na serikali.

Kupitia ufadhili wa Sh. bilioni 13.2 kutoka Shirika la Umoja wa Ulaya (EU) mradi huo utatekelezwa katika Manispaa ya Kigoma, Uvinza na Kigoma ujiji nchini Tanzania na Wilaya ya Mpululu, nchini Zambia kwa miaka minne kuanzia Septemba, 2024 hadi Augusti 2028, nchini Tanzania na Zambia.

Akiutambulisha mradi huo kwa wadau wa mazingira juzi jijini Dar es Salaam, Meneja Mradi CRS Tanzania, Robert Muganzi  alisema waliamua kuelekeza  mradi huo mkoani Kigom ili kuokoa afya za wananchi zilizopo hatarini kutokana taka kuzagaa ndani ya Ziwa Tanganyika.

Alisema mradi huo  utaiwezesha serikali  kuweka mifumo ya kisheria wa usimamizi wa taka, ili kuwa  thabiti ikiwamo kuwabana wazalishaji  waweke  mifumo mizuri ya kuzikusanya na kuzichakata.

Kupitia mradi huo wakulima na wafugaji watafundishwa mbinu endelevu  endelevu za kufanya shughuli zao bila kuathiri maji katika ziwa hilo  na kujiepusha na kukata miti,uharibifu wa udongo na  uvuvi haramu.
“Tunawafundisha kujiepusha na kilimo ambacho kinasababisha udongo uliopo kando ya ziwa kuingia ziwani na kuharifu chanzo cha maji,” alisema.

Alisema pia watatoa fedha kwa vikundi vya kinamama vya kuweka na kukopa maarufu VICOBA na kuwapatia elimu ya urejeshaji wa taka, ili kuwapa maarifa na mtaji wa kuandisha biashara hiyo.

Msingi mkuu wa mradi huo ni kujenga uelewa wa pamoja na kufanya ushirikishaji wa wadau katika utekelezaji wa mradi, na utazingatia ushirikishaji katika ngazi zote kuanzia vikundi vya kijamii, taasisi binafsi na serikali.
Ofisa Programu wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Letizia Beltrame, alisema mradi huo ni muhimu katika maendeleo ya jamii  katika nchi hizo zinazozungukwa na Ziwa Tanganyika kwa kuwa itaongoeza umakini katika usimamizi wa maji.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Ecohub, inayojishughulisha na urejeleshaji taka, Sarah Pima aliwapongeza CRS na Caritas kwa kuratibu mradi huo kwani utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha maji ya Ziwa Tanganyika hivyo kulinda afya za watumiaji.

Alipongeza pia EU kwa kufadhili mradi huo kwani uchumi rejeshi bado ni jambo jipya nchini kwa hivyo utekelezwaji wa mradi huo utaongeza maarifa na ajira, kuhifadhi mazingira, kukuza uchumi wa mtu mmoja hadi  pato la taifa.

“Kubwa nilichokipenda katika mradi huu ni namna utakavyoshirikisha makundi mbalimbali, hili ni la muhimu sana kwa kuwa utekelezwaji wa uchumi rejeshi unahitaji ushirikiano katika ngazi zote  kama jamii, sekta binafsi, wafanya uamuzi, wasomi na asasi za kiraia,”alisema Sarah.