Mkurugenzi wa DIB aitwa na mahakama

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 05:28 PM Oct 17 2024
Nyundo ya Mahakama.
Picha:Mtandao
Nyundo ya Mahakama.

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemwamuru Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB), Isaack Kihwili, kufika mahakamani kueleza hali ya utekelezaji wa amri ya Mahakama kuhusu malipo ya Sh bilioni 145 kwa Kampuni ya Coast Textile Limited.

Kihwili alipaswa kufika mahakamani jana Jumatano, lakini hakuweza, jambo ambalo lilizua mabishano kutoka kwa mawakili wanaowakilisha pande hizo mbili kuhusu kutofika kwake mahakamani.

Wakili wa Serikali Edwin Wediro,  amemweleza Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mary Moyo, kuwa Kihwili aliitikia wito wa mahakama na alikuwa mahakamani tangu asubuhi kabla ya kuondoka katika eneo hilo kwa ajili ya majukumu mengine ya kikazi.

Wakili Joseph Rutabingwa, wa Coast Textile Limited, amekanusha hoja hiyo, akidai kuwa utaratibu unaojulikana unamtaka Mkurugenzi wa DIB kufika mahakamani na si kuzunguka kwenye maeneo nje ya Mahakama.

Amedai kuwa Mahakama hiyo ilitoa amri hiyo na yeye binafsi alimpelekea Kihwili na akaipokea, kwa hiyo alitakiwa afike mbele ya mahakama, " Lakini hayupo hapa, hii ni sawa na kutotii agizo la mahakama,”.

Naibu Msajili amebaini kutokuwepo kwa Mkurugenzi wa DIB na kuagiza wahusika kufika mbele ya Jaji Mfawidhi kwa ajili ya kusikiliza shauri hilo, Oktoba 30, 2024. Jaji Salma Maghimbi ndiye anayesikiliza shauri hilo.

Katika kikao cha Mahakama kilichopita, Wakili wa Serikali ameieleza mahakama kuwa Serikali ya Marekani imeahidi kufikia Desemba 2024 kuziachia fedha zinazomilikiwa na FBME Bank Limited inazozishikilia na wadai wote, ikiwemo Kampuni ya Coast, ambayo inadai Sh bilioni145 kulingana na amri ya mahakama iliyotolewa takriban miaka tisa iliyopita, watalipwa.

Ameeleza kuwa Mkurugenzi wa Cyprus aliwasiliana na Ubalozi wa Marekani juu ya uwezekano wa kuondoa vikwazo vya fedha za Benki ya FBME, ambazo zilikuwa zikizuiwa na mamlaka za Marekani kwa tuhuma za kuhusika katika madai ya utakatishaji fedha.

Amefafanua zaidi kuwa Mkurugenzi wa DIB na Mfilisi wa Benki ya FBME nchini Cyprus walifanya kikao kujadili masuala mbalimbali, ikiwa ni pamoja na maendeleo ya mchakato wa ufilisi.

Wakili wa Serikali ameieleza mahakama kuwa kundi la wateja walioweka amana kwenye benki hiyo katika asilimia 70 ya madai iliyobaki litalipwa ifikapo Septemba, 2024. Hata hivyo, alieleza kuwa Coast Textile Limited haitakuwa miongoni mwa wanufaika katika orodha ya mwezi Septemba.

Kampuni ya Coast Textiles Ltd imeamua kuomba mahakama kuingilia kati baada ya FBME, ambayo shughuli zake zilichukuliwa na BoT, kushindwa kutekeleza hukumu iliyotolewa na Jaji Aloysius Mujulizi mwaka 2015 kuhusu malipo hayo.

Kampuni hiyo ilifungua maombi ya kukazia hukumu hiyo, ikiomba Sh. Bilioni 145.94 ipatikane kutoka kwa DIB, wafilisi wa FBME, ambapo Mkurugenzi wa Bodi akishindwa kulipa atalazimika kuwajibishwa.