Naibu Rais alazwa Hospitali ya Karen kwa maumivu ya kifua

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 06:57 PM Oct 17 2024
Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua.
Picha: Mtandao
Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua.

NAIBU Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua imeelezwa ameugua ghafla na kulazwa katika Hospitali ya Karen jijini Nairobi baada ya kupata maumivu ya kifua.

Taarifa ya kuugua kwa kiongozi huyo imetolewa leo Oktoba 17, 2024 wakati Bunge la Seneti likiendelea kujadilili hatima ya mashtaka 11 yanayomkabili, ili kuidhinisha au kubatilisha kuondoshwa kwake katika ofisi ya Naibu Rais wa Kenya.

Akilithibitishia Bunge hilo la juu hali ya Gachagua jioni ya leo Oktoba 17,2024 Wakili Mwandamizi, Paul Muite amesema kuwa Naibu Rais Rigath Gachagua baada ya kuugua ghafla alipelekwa hospitalini wakati wa shughuli ya mapumziko ya mchana katika kesi yake ya kuondolewa madarakani katika Seneti. 

Akimuelezea Spika wa Seneti Amason Kingi, Muite ambaye ni Wakili kiongozi anayemwakilisha Gachagua, alithibitisha kuwa Naibu Rais huyo aliugua na kulazimika kukimbizwa hospitalini.

 Muite alimwomba Spika Kingi ampe muda wa saa moja au mbili kumtembelea Gachagua na kutafakari iwapo anaweza kuendelea na kesi hiyo.

Gachagua alitazamiwa kutoa kauli yake na kuhojiwa na mawakili wanaowakilisha Bunge la Kitaifa. 

"Samahani na masikitiko kwamba Naibu Rais hayupo na usumbufu na ucheleweshaji uliosababishwa kwa Spika na Seneta. Msimamo ni kwamba katika kipindi kile tulichoenda nilijaribu kujua kwanini hayupo, ukweli wa kusikitisha ni kwamba. Naibu Rais amechukuliwa akiwa mahututi na yuko hospitalini," Muite amesema. 

Kutokana na hatua hiyo Spika wa Seneti Amason Kingi ameahirisha kesi ya kumwondoa Naibu Rais Rigathi Gachagua baada ya shahidi huyo muhimu kutokuwepo kwaajili ya mahojiano ya moja kwa moja na mawakili upande wa Bunge. 

Aidha, Wakili Muite ameahidi kuleta ripoti kufikia saa kumi na moja jioni juu ya hali ya mteja wake na kama angeweza kuendelea na hatua hiyo au la.

Hata hivyo, awali Wakili wa Bunge, alipingana na hoja hiyo na kumtaka Spika kuendelea na shauri hilo bila kuwapo kwa DP Gachagua kwa kuwa ni mchakato wa muda unaopaswa kukamilika siku hiyo.

 Baada ya kukagua hoja zote mbili, Spika Kingi aliamua kwamba kikao cha Seneti kingesitishwa hadi saa kumi na moja jioni.

 "Baada ya kuzingatia pande hizo mbili, maelekezo yangu ni kama ifuatavyo: kwamba tusitishe kikao hiki na turudi saa kumi na moja jioni. Tunatarajia DP kuchukua nafasi ya mashahidi. Huu ni mchakato unaozingatia wakati kwa bahati mbaya imeamriwa," Kingi aliamua.