Mashahidi 36, vielelezo 116 katika kesi ya aliyekuwa Mkurugenzi TPA

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 07:47 PM Oct 17 2024
Mashahidi 36, vielelezo 116 katika  kesi ya aliyekuwa Mkurugenzi TPA
Picha: Mtandao
Mashahidi 36, vielelezo 116 katika kesi ya aliyekuwa Mkurugenzi TPA

UPANDE wa Mashtaka, unatarajia kuwa na mashahidi 36 na vielelezo 116 katika usikilizwaji wa kesi inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Madeni Kipande na wenzake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Hata hivyo, upande huo ulimuondolea mashtaka Peter David ambaye alikuwa miongoni mwa washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi yenye mashtaka matatu likiwemo la matumizi mabaya ya madaraka.

Washtakiwa wengine waliyobaki katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa Idara ya Manunuzi, Mashaka Kisanta , Mwenyekiti wa Bodi ya Manunuzi, Casmily Lujegi na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Kilian Chale na Endrew John.

Taarifa hiyo ilitolewa juzi na jopo la mawakili watano wa Serikali akiwemo Nickson Shayo na Winiwa Kasala mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu wa Mahakama hiyo, baada ya kumaliza kuwasomea washtakiwa maelezo ya mashahidi (Committal proceedings).

 Baada ya washtakiwa kusomewa maelezo hayo, jarada la kesi hiyo litahamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa mashahidi.

 Katika kesi hiyo, Kipande na wenzake wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuongoza genge la uhalifu, matumizi mabaya ya mamlaka na kuisababishia mamlaka hiyo hasara.

 Ilidaiwa kati ya Januari Mosi na Februari 17 , 2015, wakiwa maofisa wa TPA, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutangaza zabuni namba AE/016/2014-15/CTB/G/39 kwa nia ya kujipatia Dola za Marekani 1,857,908.04 .

 Inadaiwa kati ya Oktoba Mosi, 2014 na Oktoba Mosi, 2020 maeneo ya TPA na maeneo mengine ya Dar es Salaam, kwa makusudi walitangaza zabuni ya Enterprises Planning Resources (ERP).

 Washtakiwa hao wanadaiwa walitangaza zabuni hiyo, bila kupata kibali cha Bodi ya zabuni ya mamlaka hiyo na kushindwa kufuata kanuni za zabuni, hivyo kutoa malipo ya awali ya asilimia 40 bila idhini ya Bodi hiyo, jambo lililosababisha TPA kupata hasara ya Dola za Marekani milioni 1.8.