Shydc wafanya bonanza kuhamasisha uandikishaji daftari la wakazi

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 06:05 PM Oct 17 2024
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk.Kalekwa Kasanga akizungumza kwenye Bonanza hilo.
Picha: Marco Maduhu
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk.Kalekwa Kasanga akizungumza kwenye Bonanza hilo.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Shinyanga imefanya bonanza la michezo, kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wakazi.

Bonanza hilo la michezo limefanyika leo Oktoba 17,2024  katika Stendi ya Mabasi Salawe,ambalo limeongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Dk.Kalekwa Kasanga.

Dk.Kasanga akizungumza wakati wa ufunguzi wa bonanza hilo la michezo, amewasihi wananchi wa Wilaya ya Shinyanga kwamba, waendelee kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la wakazi, ili wapate fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 27 mwaka huu.

"Siku za kujiandikisha kwenye daftari la wakazi zimebaki 3 ambalo lilianza Oktoba 11 na litatamatika tarehe 20 nawaombeni wananchi mjitokeze kujiandikisha ili mtumie haki yenu ya kikatiba kupiga kura na kuchagua viongozi wazuri watakao waletea maendeleo," amesema Dk.Kalekwa.

Diwani wa Salawe Joseph Buyugu, naye amewasisitiza wananchi kwa wale ambao bado hawajajiandikisha, kwamba wajiandikishe kwani siku siyo rafiki,ili wasije wakashindwa kupiga kura.

Uchaguzi huo wa serikali za mitaa ambao utafanyika Novemba 27 mwaka huu, ni kuchagua wenyeviti wa vijiji,vitongoji,mitaa pamoja na wajumbe.