Profesa Sedoyeka ajitetea mbele ya Baraza la Maadili

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 07:39 PM Oct 17 2024
MKUU wa Chuo katika Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamini Sedoyeka.
Picha:Mtandao
MKUU wa Chuo katika Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamini Sedoyeka.

MKUU wa Chuo katika Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamini Sedoyeka ametumia zaidi ya saa tatu kutoa utetezi wake kwa Baraza la Maadili katika tuhuma nne zinazomkabili na kwamba katika utekelezaji wa majukumu yake siku zote ametanguliza maslahi ya chuo na taifa.

Utetezi huo aliutoa leo Oktoba 17,2024 kwenye kikao cha baraza hilo jijini hapa chini ya Mwenyekiti wa Baraza Jaji Mstaafu Rose Teemba na upande wa mlalamikaji uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali Emma Gellan na Hassan Mayunga.

Sedoyeka anadaiwa kukiuka maadili ya viongozi ya umma kwa kumpandisha cheo mtumishi kwa upendeleo,  kuingilia mchakato wa ununuzi wa viti na meza kampasi ya Babati na uhusiano wa karibu na mtumishi na kufanya uhamisho wa ndani wa mtumishi.

Akitoa utetezi wake, Prof. Sedoyeka amesema hakuwa na mamlaka ya kumpandisha cheo cha kitaalum mtumishi Hakimu Ndatama na alichofanya ni uteuzi wa kumpatia majukumu ya kuwa mkuu wa sehemu na sio Mkuu wa Idara ya Rasilimali watu ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji.

Kuhusu kuwa na uhusiano wa karibu na mtumishi huyo, Prof. Sedoyeka amesema hajahusika kwa namna yeyote kumrejesha Hakimu kwenye chuo hicho kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo awali alihamia na kuwa Msaidizi wa Katibu Mkuu wakati akitumikia nafasi ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.

“Mimi niliripoti Machi 13, 2023 niliporudishwa IAA lakini barua ya Hakimu kuomba kutoka Wizara ya Maliasili na kurudishwa IAA ilitolewa Machi 9, 2023,” amesema.

Akizungumzia tuhuma ya kuingilia mchakato wa zabuni, Prof. Sedoyeka alifafanua kuwa dhana iliyokuwa imejengeka chuoni hapo ni kutumia mzabuni mmoja, lakini akiwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu alijifunza kuwa zabuni inafanywa kwa ushindani na kuna kampuni nyingi zinazoweza kutoa huduma bora zaidi na kwa bei nafuu.

Amesema katika zabuni hiyo kuna wazabuni ambao walitoa bei nafuu kuliko ambaye alikuwa amepitisha ambaye ni kampuni ya Jaffer na bei yake kwa kiti na meza ni Sh. 440,000 huku Timber ilikuwa Sh.389,000 na Vadeck ni Sh.346,000.

“Nilipokuta mwenye gharama kubwa ameshinda ndipo nikafuatilia mchakato wa hii zabuni, nilibaini viliwekwa vigezo maalum vya bidhaa hiyo na maelezo ya tathmini iliyofanywa na kamati ya manunuzi ilifafanua kwenye bidhaa ya kampuni moja huku kukiwa hakuna maelezo ya kampuni zingine,” amesema.

Kuhusu kumhamisha mtumishi wa Idara ya Ugavi, Robert Mwintango (Afisa Ugavi) kumpeleka maktaba, amesema alifanya kwa nia njema na ni uhamisho wa kawaida wenye kuongeza ufanisi kwenye kitengo husika.

“Ni kawaida idara yenye wafanyakazi wengi kwenda kusaidia idara zenye upungufu wa watumishi, wakati na mhamisha Robert idara yao ilikuwa na watumishi 10, lakini pia maktaba hawakuwa na mtu wa manunuzi na wakati huo kulikuwa na ununuzi mkubwa na kulikuwa na matumizi ya mfumo mpya wa manunuzi wa NeST. Hivyo nilifanya uhamisho wenye nia njema na alipomaliza lile jukumu alirudi kwenye Idara ya manunuzi,”amesema.

Aidha, ameomba baraza hilo lisimtie hatiani kwenye tuhuma hizo na kwamba anafanya kazi kwa hali na nguvu ili kuleta mafanikio kwenye taasisi hiyo na hakuwa na nia ovu na ataendelea kuitumikia IAA.

Akihitimisha kikao hicho, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji Teemba amesema wamepokea ushahidi wa pande zote mbili na baraza limekamilisha kazi yake na baada ya uchambuzi litawasilisha taarifa yake sehemu husika.