15,000 waitwa usaili wa walimu nafasi 11,000

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 11:18 AM Oct 17 2024
15,000 waitwa usaili wa walimu nafasi 11,000
Picha:AI
15,000 waitwa usaili wa walimu nafasi 11,000

MAELFU ya waombaji nafasi za kazi za ualimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wameitwa kwenye usaili kwa ajili ya ajira 11,000 ambao unatarajiwa kuanza Oktoba 23, mwaka huu.

Julai mwaka huu, serikali ilitangaza nafasi hizo za kazi za walimu wa shule za msingi na sekondari.

Awali,  waombaji wa kada hiyo walikuwa wakiomba kupitia mfumo wa ajira wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na hakukuwa na usaili wa aina hiyo. Waombaji walikuwa wakiomba kwenye mfumo huo na baada ya uchambuzi, wenye sifa walikuwa wakipangiwa vituo vya kazi.

Hata hivyo, nafasi hizo za ajira safari hii jukumu limefanywa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma.

Katika tangazo lililotolewa na sekretarieti hiyo la kuwaita kwenye usaili waombaji linabainisha kuwa usaili huo utaendeshwa kuanzia Oktoba 23 hadi Novemba 16, mwaka huu na hatimaye kuwapangia vituo vya kazi kwa watakaofaulu.

Ratiba ya usaili wa mchujo itakuwa Oktoba 23, mwaka huu, saa 1:00 asubuhi kwa walioomba ualimu daraja la IIIA na elimu ya awali na utafanyika kwenye vituo mbalimbali kulingana na anwani ya mwombaji ya sasa.

Novemba 11 hadi 16, mwaka huu utafanyika usaili wa mahojiano kwa waombaji wa nafasi hizo kwenye mikoa ambayo wasailiwa walichagua na kuthibitisha kuwa wameomba kazi katika mkoa huo na kwamba vituo husika watajulishwa kupitia akaunti zao za Ajira Portal na tovuti ya sekretarieti hiyo.

Pia kwa upande wa nafasi ya Mwalimu Daraja la IIIB somo la Bailojia, Kemia, Jiografia na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), usaili wa mchujo utafanyika Oktoba 25, mwaka huu, saa 1:00 asubuhi kwenye vituo mbalimbali kulingana na anwani za sasa za waombaji husika.

Katika usaili wa mahojiano kwa nafasi hizo, kwa Novemba 13, mwaka huu, saa 1:00  asubuhi utafanywa kwa nafasi ya Mwalimu daraja IIIB wa somo la Bailojia na Kemia huku Novemba 15 itakuwa mwalimu wa daraja hilo wa Jiografia na Novemba 18 Mwalimu wa TEHAMA.

Kadhalika, usaili wa mchujo kwa Mwalimu daraja IIIB wa Historia, Shule za Msingi, Kiswahili, Elimu ya Awali, Uraia watafanyiwa usaili Oktoba 27, mwaka huu, na usaili wao wa mahojiano utafanyika kwa mwalimu wa Historia Novemba 15, mwaka huu, Kiswahili, Uraia na Elimu ya Awali (Novemba 16) na Mwalimu wa Shule ya Msingi (Novemba 19).

Oktoba 31, mwaka huu, utafanyika usaili wa mchujo wa nafasi ya Mwalimu wa Daraja IIIC wa Jiografia na usaili wa mahojiano utafanyika Novemba 15.

 Novemba 2, utafanyika usaili wa mchujo nafasi ya Mwalimu wa Daraja la IIIC wa Historia na usaili wake wa mahojiano utakuwa Novemba 15. Nafasi ya Mwalimu wa Fasihi ya Kiingereza daraja la IIIC usaili wa mchujo na mahojiano utakuwa Novemba 16, mwaka huu.

Hata hivyo, usaili wa mchujo kwa Mwalimu daraja la IIIC wa Somo la Baiolojia, Tehama, Uchumi utafanyika Novemba 6, mwaka huu, wakati wa mahojiano utakuwa Novemba 14 kwa Mwalimu wa Baiolojia, Novemba 15 Mwalimu wa Uchumi na Novemba 18 Mwalimu wa TEHAMA.

 Usaili wa Mchujo kwa Mwalimu daraja la IIIC wa Somo la Kemia, Shule za Msingi, Elimu Maalum, Uraia na Kilimo utakuwa Novemba 8, mwaka huu, huku usaili wa mahojiano utakuwa Novemba 13 utakuwa kwa Mwalimu wa Kemia, Uraia (Novemba 16), Kilimo (Novemba 18), Shule za Msingi na Elimu Maalum (Novemba 19).

Aidha, waombaji wa Mwalimu daraja la IIIB wa Fizikia wao watafanya usaili wa mahojiano Novemba 14, mwaka huu huku Mwalimu wa daraja IIIB wa Hisabati utafanyika Novemba 12, mwaka huu sambamba na Mwalimu daraja IIIC wa Fizikia na Hisabati.

 Kwa Mwalimu wa Fasihi ya Kiingereza daraja la III B, usaili  utafanyika usaili wa mahojiano Novemba 16, mwaka huu na Novemba 18 utafanyika kwa waombaji wa Mwalimu daraja la IIIB wa Kifaransa, Somo la Biashara, Lishe, Ushonaji na Kilimo sambamba na Mwalimu daraja la IIIC wa somo la Biashara na Maabara.

Novemba 19, utafanyika wa usaili wa mahojiano kwa nafasi ya Mwalimu elimu maalum IIIA, Mwalimu daraja IIIB Somo la Biashara, Elimu maalum na Mwalimu wa daraja IIIC somo la Biashara.

 Hivi karibuni, Naibu Waziri  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu alisema kuwa azma ya serikali ya kupeleka kibali cha ajira kwa kada za afya na elimu katika Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni kuhakikisha serikali inapata watumishi wenye sifa, ili kuongeza tija na ubora katika utumishi wa umma.

Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa usaili huo utaendeshwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu.