Yanga yahamishia hasira kwa Al Hilal

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:53 AM Nov 17 2024
Kocha mpya Mjerumani, Sead Ramovic.
Picha: Mtandao
Kocha mpya Mjerumani, Sead Ramovic.

SIKU moja baada ya kumtangaza kocha mpya Mjerumani, Sead Ramovic, uongozi wa Yanga umetamba wanajipanga kulipa kisasi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal kutoka Sudan itakayochezwa Novemba 26, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara walisema haiwezekani timu yao kufungwa mechi tatu mfululizo na mashindano mbalimbali.

Yanga imeapa kumaliza hasira za kuondolewa na Al Hilal katika mashindano ya CAF mwaka juzi, lakini pia ikitaka kurejesha furaha kwa mashabiki wao ambao wanaugulia kufuatia kuruhusu kufungwa bao 1-0 na Azam na kichapo cha magoli 3-1 kutoka kwa Tabora United, mechi zote za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza jijini jana, Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema kitendo cha kufungwa mara mbili kimewahuzunisha wanachama, mashabiki na wapenzi wa klabu yao, hivyo kwa vyovyote hawawezi kukubali kupoteza mechi nyingine ya tatu lakini ya kwanza kwenye hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Tumepoteza mechi mbili mfululizo, hatutakubali tena kupoteza mchezo mwingine wa tatu. Huu ni mchezo muhimu kwetu, ni lazima tushinde turudi kwenye njia yetu tulioizoea, hatuwezi kukubali klabu kubwa kama Yanga ifungwe michezo mitatu mfululizo kwa sababu kizazi chetu kitakuwa kimeingia katika rekodi mbaya sana tangu kuanzishwa kwa klabu hii," alisema Kamwe.

Ofisa huyo aliongeza chini ya kocha mpya wanatarajia mambo mazuri na Yanga haitasikiliza 'kelele' za wachambuzi kufuatia uamuzi wake wa kuachana Miguel Gamondi.

"Hautasikia uongozi wa Yanga unajibu lolote kuhusiana na uamuzi wa kuachana na Gamondi, yalisemwa mengi wakati tunaachana na Nabi (Nasreddine), tuliambia tumeleta kocha ambaye alikuwa hana kazi kwa miezi sita.

Angalieni (German mashine- Ramovic), ameondoka kwa sababu gani, tunaendelea na mipango yetu ili kufikia malengo, tunatakiwa kuwa na mbinu mpya pale ambapo timu inahitaji kusonga mbele, tumeshatwaa ubingwa mara tatu, sasa tunataka kuendelea hadhi hii, ni lazima tuje tofauti," alisema Kamwe.

Aliongeza kocha huyo mpya ameshakutana na wasaidizi wake tayari kuanza mipango kwa ajili ya kuelekea mechi yao ya kimataifa na wanawaomba mashabiki wafike uwanjani wakiwa wamevalia jezi mpya ambazo zinatarajiwa kuzinduliwa Jumatano.

"Kocha wetu baada ya kutangazwa hapo jana (juzi) aliita kikao na wasaidizi wake, Mjerumani huyu hana kupoa kafika tu kataka kikao kingine kwa ajili ya kuhakikisha tunakwenda sawa kwenye maandalizi ya timu yetu kuelekea mechi dhidi ya Al Hilal.

Nitumie fursa hii kuwaambia wanachama, mashabiki na wapenzi wa Yanga jezi zetu tayari zimefika na zitazinduliwa Novemba 20, mwaka huu, tunataka wakati watu wananunua tiketi basi, na jezi pia ziwe tayari sokoni zinauzwa.

Mechi itapigwa kuanzia saa 10:00 jioni, tunaamini ni muda ambao mchezo utaisha mapema ili watu warejee majumbani mapema kwa ajili ya kuamkia kazini Jumatano," alisema Kamwe.

Ofisa huyo alikanusha klabu yao kumwajiri aliyekuwa Kocha Mkuu wa KMC FC,  Abdihamid Moallin, na kuongeza kocha wao msaidizi atatangazwa wakati wowote kuanzia sasa.

"Mmendika kuhusu Moallin, si kweli, hakuna ukweli, nawaambia leo (jana),  naua hizo tetesi na taarifa, na Wanayanga wote ambao waliamini hiki kitu nawaambia rasmi si kweli, hakuna ambaye amewahi kumwona kocha wetu msaidizi, hakuna yoyote anayejua jina lake wala ubini wake, yupo hapa hapa nchini, hajui kiswahili la kingereza, anajua lugha ya kwao Poland tu," Ofisa habari huyo aliongeza.

Hata hivyo bado haijafahamika Moallin ambaye amebwanga manyanga ya kuifundisha KMC atajiunga na timu gani baada ya Gamondi kutimuliwa na msaidizi wake, Moussa Ndaw.

Tayari KMC imemtangaza, Kalimangonga Ongalla, ambaye aliwahi kufanya kazi Azam FC kuwa kocha mpya.