Wenye maumivu watatuliwa shida yao ya kudumu

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 06:04 PM Nov 14 2024
ed Janabi
Christina Mwakangale
ed Janabi

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH), imefanya upasuaji kwa wagonjwa 25 kati ya 186 wenye maumivu sugu kwa kusitisha (ku-block) mshipa wa fahamu unaoleta hisia za tatizo hilo na kuwaondoa kwenye hatari ya kupata tatizo la figo na magonjwa ya akili.

Kwa mujibu wa MNH, hupokea magonjwa wenye maumivu wapatao 40 wakifikia takribani 200 kwa wiki huku ikikadiriwa 800 ndani ya mwezi mmoja, wengi wao wakisumbuliwa na maumivu ya mgongo.

Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi, akizungumza na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam, alisema wagonjwa hao wenye maumivu ya muda mrefu walilazimika kutumia dawa za kutuliza tatizo hilo kila siku na kuathiri afya ya akili.

Alisema maumivu haya ambayo ni makali yanaweza kusababishwa na mambo kadhaa kama vile kudhoofika kwa viungo vya mwili kutokana na umri, tatizo la saratani, majeraha kutokana na ajali, athari za upasuaji, magoti na mabega.

“Ukiwa na maumivu sugu na makali huwezi kukimbia, kulala kama una maumivu ya bega moja au mgongo, utalalia upande mmoja. MNH katika idara ya radiolojia tuna wataalamu ambao wanatoa huduma aina hiyo.

“Kwa kipindi cha siku 10 tumewaona wagonjwa takribani 200 na 25 wametibiwa na kuwapatia matumaini mapya ya maisha bora. Ni huduma mpya nchini,” alisema Prof. Janabi.

Alisema kwamba miongoni mwa athari kuu nne zinazosababishwa na utumiaji holela wa dawa za kutuliza maumivu kwa muda mrefu, ni figo kushindwa kufanya kazi zake.

Profesa David Prologo kutoka hospitali ya Emory Johns Creek nchini Marekani, alisema amefika MNH, ili kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani na kisha kuifanya huduma hiyo kuwa endelevu.

“Uwekezaji ulioko hapa MNH umefanikisha huduma kufanyika na idara ya radiolojia ina vifaa vizuri kimataifa. Huduma hii imesaidia wagonjwa ambao hawana mbadala wa tiba na kuishi na maumivu maisha yote,” alisema Prof. Prologo.

Bingwa Mbobezi wa Radiolojia na Mkuu wa Idara ya Radiolojia MNH, Dk. Fredrick Lyimo, alisema matibabu aina hiyo hufanyika kwa kufanya upasuaji wa tundu dogo kwenye tatizo na kukata mawasiliano ya mfumo wa fahamu unaosababisha mtu ahisi maumivu.