Polisi wamshikilia Mbuya tuhuma mauaji ya Baba mkwe wake

By Mary Mosha , Nipashe
Published at 08:08 PM Nov 14 2024
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa.

JESHI la Polisi linamshikilia Deogratias Mbuya (40) makazi wa Legho Kilema, Wilaya Moshi mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kumuua Baba mkwe wake aliyejulikana kwa jina Tibrus Mneney (72) baada ya kushindwa kutatua mgogoro wa ndoa.

Tukio hilo lilitokea jana Novemba 13,2024  katika Kijiji cha Legho Kilema, wakati wa kikao cha familia cha usuluhishi baina ya mtuhumiwa na mkewe, kilichokosa suluhu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amethibitisha tukio hilo, akieleza kuwa ugomvi ulianza baada ya mtuhumiwa kuanza kumshambulia mama mkwe wake, Biritha Mneney (58), na baba mkwe aliingilia kati. Mtuhumiwa alimjeruhi Tibrus kwa kumkata na kitu chenye ncha kali shingoni, kichwani, na mkononi, na kusababisha kifo chake kutokana na kuvuja damu nyingi.

"Mtuhumiwa  alikuwa na mgogoro  wa ndoa na mkewe akimtuhumu kutoka nje ya ndoa mara baada ya kufanyiwa upasuaji kutokana na matatizo ya kiafya. Baada ya kushindwa  kupata suluhisho alianza kumpiga mama mkwe( Biritha  Mneney (58 ) ndipo baba mkwe (Tibrus Mneney) alipoingilia kati na kuanza kukatwa katwa ,"alisema Kamanda.

Kamanda amesema , mara baada ya  mtuhumiwa  kutekeleza tukio hilo,  alitoroka na msako mkali uliendelea  hadi leo Novemba 14 alipokutwa kwenye nyumba bovu ya  Revocatus Mbuya akiwa hawezi kuongea  na kueleza hivi sasa amelazwa katika Hospitali ya rufaani ya kanda KCMC  kwa uchunguzi na matibabu zaidi.