ALIYEKUWA Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Lawrence Mafuru, amefariki kwa ugonjwa wa saratani ya damu, baada ya kuugua kwa muda mfupi, imeelezwa.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk. Tausi Kida, amesema leo kwamba Mafuru alianza kuugua miezi mitatu iliyopita na kupata matibabu katika hospitali ya Taifa Muhimbili, kisha kuhamishiwa Appolo nchini India.
Ameyasema hayo leo Novemba 14, jijini Dar es Salaam, alipokuwa akisoma wasifu wa marehemu, wakati wa ibada maalumu ya kuaga mwili wa Mafuru, ambaye alifariki Jumamosi iliyopita, akiwa nchini India.
“Alianza kuugua Agosti 2024, akaanza kuhudumiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili na baadaye akapelekwa hospitali ya Appolo nchini India, kwa matibabu zaidi. Alifariki Novemba 09, 2024 akiwa na umri wa miaka 52,” amesema.
Amesema Mafuru alizaliwa Juni 20, 1972 mkoani Mara na kusoma shule za msingi na sekondari hapa nchini, kisha kujiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi ngazi ya shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara.
Amesema amefanyakazi sekta binafsi kwenye benki kadhaa hadi mwaka 2016, alipoteuliwa kwenye utumishi wa umma, akiwa Msajili wa Hazina.
Katika ibada hiyo ya kitaifa, iliongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Jimbo la Kaskazini mwa Tanzania, Mchungaji Mark Malekana, ambaye alisoma neno la faraja kutoka kitabu cha Zaburi ya 90:1-3.
Ibada hiyo imehudhuriwa na viongozi waandamizi wa serikali, sekta binafsi na wastaafu, wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Viongozi wengine ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Spika, wafanyabiashara, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED