MUHAS yapokea ruzuku ya bilioni 12.5 kutoka Sweden kwa mafunzo na utafiti wa afya

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:47 PM Nov 14 2024
MUHAS yapokea ruzuku ya bilioni 12.5 kutoka Sweden kwa mafunzo na utafiti wa afya

Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kimepokea ruzuku ya shilingi bilioni 12.5 kutoka kwa Shirika la Maendeleo la Sweden (SIDA) kwa ajili ya kufundisha wataalam wa afya katika ngazi za Shahada ya Uzamili na Uzamivu, pamoja na kuboresha utafiti na uvumbuzi nchini.

Ruzuku hiyo, inayotarajiwa kudumu kwa miaka sita kuanzia Desemba 2024 hadi Juni 2030, inalenga kukuza ubunifu na kuchangia maendeleo ya sekta ya afya nchini Tanzania.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini ya mkataba huo, Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema ushirikiano wa MUHAS na Sweden ulianza mwaka 1980 na umeendelea kuwa na mafanikio makubwa, ikiwemo kuboresha miongozo na sera za afya nchini.

Prof. Kamuhabwa ameongeza kuwa MUHAS itashirikiana na vyuo vikuu vya Umeå, Karolinska, na Uppsala vya Sweden, ambapo wanafunzi watakaofaidika watapata nafasi ya kujifunza na kufanya utafiti katika vyuo hivyo.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Bruno Suguya, ameeleza kuwa ruzuku hiyo itasaidia utafiti kwenye magonjwa kama malaria, kifua kikuu, huduma za mama na mtoto, na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi. 

Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Dk. Harrison Mwakyembe, amesifu juhudi za MUHAS katika kutoa ufumbuzi wa changamoto za afya kupitia utafiti.

1

Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Charlotta Ozaki Macias, amesema ufadhili huo utaimarisha uwezo wa MUHAS katika kutatua changamoto za sekta ya afya kwa kutumia mbinu za kisasa.

Wakati huo huo, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, ameeleza kuwa serikali imewekeza trilioni 6.2 kuboresha sekta ya afya kwa kujenga miundombinu na kununua vifaa tiba vya kisasa, huku akiangazia umuhimu wa utafiti na utaalamu katika huduma za afya.