Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, serikali imetumia shilingi trilioni 6.2 kuboresha sekta ya afya nchini.
Akizungumza kuhusu maendeleo hayo, Mhagama alisema kuwa uboreshaji huo umejumuisha ujenzi wa miundombinu, ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa, pamoja na vifaa vya uchunguzi na dawa, hatua ambazo zimewezesha huduma za afya kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Mhagama ameyasema hayo leo wakati wa ufunguzi wa kongamano la kidigitali katika sekta ya Afya lililofanyika eneo la Mloganzila.
Waziri Mhagama ameongeza kuwa Chuo cha MUHAS kinatoa wataalam wabobezi ambao wamechangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha huduma za afya nchini.
Ameeleza kuwa kwa kujenga miundombinu imara na kununua vifaa tiba vya kisasa, Tanzania inasaidia kuhakikisha huduma bora za afya, kuanzia uchunguzi hadi matibabu, zinapatikana kwa wananchi wote.
Akigusia ushirikiano na Sweden, Waziri Mhagama ameeleza kuridhishwa na teknolojia inayotumika nchini humo ambayo hutoa taarifa za viashiria vya saratani ya matiti na kizazi kwa wanawake.
Amesema teknolojia hiyo inatoa taarifa sahihi kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali na kuwa Tanzania imejipanga kutumia teknolojia hiyo ili kuboresha huduma za awali kwa wagonjwa wenye viashiria vya saratani.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED