Waziri Lukuvi aeleza maono ya Isimani ijayo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:44 PM Nov 14 2024
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) William Lukuvi.
Picga:Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) William Lukuvi.

IMEELEZWA kwamba mpango wa kuchimba mabwawa ya kuhifadhi maji kwa ajili ya matumizi ya shughuli za kilimo kwa wananchi wa Tarafa ya Isimani utachangia kukuza fursa za uchumi na kuimarisha kipato cha wananchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) William Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Isimani wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Isimani katika Kata ya Kising’a jana.

Alifafanua kwamba miradi ya maji safi imefanikiwa kutokana na fedha zilizotolewa na serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kusaidia kupatikana maji kutoka chanzo cha maji Kilolo na Maji kutoka Mtandao wa Maji Iringa Mjini kupitia Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Iringa (IRUWASA).

“Lazima tufikirie namna ya kuweka mipango ya kuhifadhi maji ili yatusaidie katika shughuliza kilimo cha umwagiliaji na yasaidie mwananchi mmoja mmoja katika kuimarisha uchumi wa wananchi wa Isimani,” alisema Waziri Lukuvi.

Ikiwa huduma zote muhimu za Maji, Barabara, Elimu, Afya Serikali imeimarisha sasa ni wakati wa kufikiria mipango endelevu itakayosaidia wananchi kuhifadhi maji ili kukabilina na hali ya ukame.

Kwa Upande wake Diwani wa Kata ya Kising’a,Rita Mlagala aliishukuru Serikali kupitia Halmashauri ya Iringa kwa kutenga kiasi kikubwa cha fedha katika mikopo ya asilimia kumi inayotolewa kwa ajili ya Vijana Wanawake na Makundi maalumu. 

Mlagala alisema,”fedha hizo zitagawawiwa kwa usimamizi mzuri kwa kuangalia vikundi vienye sifa kwa kupitia utaratibu uliowekwa na serikali wa kuwa na Kamati za Mikopo za  Kata zitakazo ratibu utoaji wa mikopo hiyo.”