EWURA yatia chachu vijana kusomea masuala ya maji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:56 PM Nov 14 2024
EWURA yatia chachu  vijana kusomea masuala  ya maji
Picha:Mpigapicha Wetu
EWURA yatia chachu vijana kusomea masuala ya maji

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewazawadia wahitimu wawili bora wa Chuo cha Maji, Florence Theonist na Emmanuel Nyaki, kompyuta mpakato na fedha Sh.Milioni tatu kila mmoja kama sehemu ya kutambua juhudi zao katika masomo na kuwahamasisha vijana wengine kujiunga na masomo yanayohusu masuala ya maji.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso  amewakabidhi wahitimu hao zawadi hizo kwenye mahafali ya 48 ya Chuo cha Maji yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. 

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa EWURA baada ya hafla hiyo, David Linda, Mhandisi Mwandamizi wa Maji na Usafi wa Mazingira amebainisha kuwa lengo la zawadi hizo ni kuhamasisha vijana wengi kujiunga na kozi za sekta ya maji ili kuwa na wataalamu wengi watakaosaidia katika kutoa huduma bora na kuchangia maendeleo ya sekta hiyo.  

Naye, Mhitimu Florence Theonest, ameishukuru EWURA kwa zawadi hiyo na kueleza kuwa kompyuta aliyopokea itamsaidia katika kazi za kiufundi, hasa ikizingatiwa kuwa shughuli nyingi za uhandisi wa maji zinategemea programu mbalimbali za kiteknolojia.