Daktari Bingwa: Ukinywa bia zaidi ya moja huathiri mfumo wa ubongo

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 05:15 PM Oct 17 2024
Dk. Mohamed Mnacho.
PICHA: MNH-Mloganzila
Dk. Mohamed Mnacho.

BINGWA Mbobezi wa Magonjwa ya Mfumo wa Fahamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk. Mohamed Mnacho anasema mtu anapokunywa pombe na kulewa, tafsiri yake ameuathiri mfumo wa uwiano katika ubongo.

Anasema mtu anapolewa na kuyumba husababisha mfumo huo kukosa uwiano (balance) na kwamba matumizi ya pombe yaliyopitiliza yanaweza kusababisha magonjwa ya mfumo wa fahamu, kwa kuwa kemikali zilizoko kwenye pombe huleta madhara.

“Athari hutokea kwenye seli za mfumo wa ‘balance’ ya ubongo na mwisho wake seli za ubongo zinaweza kufa kabisa, ataanza kupata changamoto za kusahau, kutetemeka, kuchanganyikiwa na baadaye anaweza kupata kifafa.

“Ni vizuri jamii ikajiepusha na matumizi ya pombe yaliyokithiri kwa kuwa pombe ikizidi inakuwa ni sumu na madhara yake ni ya muda mrefu na mtu akipata magonjwa haya yatokayo na athari ya matumizi ya pombe matibabu gharama. Kama ni lazima sana kunywa pombe, kunywa chupa bia moja.”