Prof. Sedoyeka asomewa tuhuma nne kwenye baraza la maadili

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:54 PM Oct 17 2024
MKUU wa Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamini Sedoyeka akiwa mbele ya kamati hiyo.
Picha: Mpigapicha Wetu
MKUU wa Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamini Sedoyeka akiwa mbele ya kamati hiyo.

MKUU wa Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamini Sedoyeka amefikishwa kwenye Baraza la Maadili kutokana na malalamiko manne ya kukiuka maadili ya viongozi wa umma.

Malalamiko hayo ni kumpandisha cheo mtumishi kwa upendeleo,  kuingilia mchakato wa ununuzi wa viti na meza, kuwa na uhusiano wa karibu na mtumishi na kufanya uhamisho wa ndani wa mtumishi kinyume na maadili ya viongozi wa umma.

Kikao cha baraza hilo kimeketi jijini Dodoma chini ya Mwenyekiti wa Baraza Jaji Mstaafu Rose Temba na upande wa mlalamikaji umewakilishwa na Mawakili wa Serikali Emma Gellan na Hassan Mayunga.

Akisoma hati ya malalamiko mbele ya Baraza, Emma amesema kuwa Prof. Sedoyeka akiwa anatekeleza majukumu yake ya uongozi pasipo kufuata Sheria kanuni na taratibu za utumishi wa umma alimpandisha cheo Hakimu Ndatama kutoka Afisa Rasilimali daraja la pili na kuwa Mkuu wa Sehemu ya Rasilimaliwatu kabla ya kukamilika kwa uhamisho wa mtumishi huyo na bila kuwa na sifa na vigezo.

Pia, amesema malalamiko mengine kuwa na uhusiano wa ukaribu na Ndatama kwa kufanya naye kazi IAA na kisha Wizara ya Maliasili na Utalii na aliporudishwa tena IAA, Mtumishi huyo aliombewa ahamie IAA mara tu baada ya mlalamikiwa kuteuliwa kuongoza taasisi hiyo.

"Jambo jingine linalolalamikiwa ni  kuingilia mchakato wa zabuni ya ununuzi na ufungaji wa viti na meza katika Kampasi ya Babati kwa kuifuta bila kufuata utaratibu na bila sababu za kisheria," amesema.

Pia, Prof.Sedoyeka anakabiliwa na malalamiko ya kufanya uhamisho wa ndani wa mtumishi Robert Mwintango (Afisa Ugavi) kutoka Kitengo cha Ununuzi na Ugavi kwenda Idara ya Maktaba tofauti na sifa za kitaaluma za mtumishi.