MAZUNGUMZO MAALUMU -3 KAMANDA MSSIKA: Atishiwa kurogwa kisa kufuatilia kesi

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 11:46 AM Oct 17 2024
Kamanda mstaafu Abdallah Mssika
Picha:Nipashe Digital
Kamanda mstaafu Abdallah Mssika

Katika sehemu ya pili jana, Kamanda mstaafu Abdallah Mssika alitaja matukio mambo manne ambayo hatoyasahau katika utumishi wake wa miaka 40 ndani ya Jeshi la Polisi, ikiwa ni pamoja na kuripotiwa isivyo sahihi na vyombo vya habari kwamba alitaka kununua cheo cha Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP).

Endelea na sehemu ya mwisho ya mazungumzo yake na Nipashe, akisimulia namna alivyokabiliana na vitisho, ikiwamo kurogwa, katika kutekeleza majukumu yake. 

--- 

KAMANDA Mssika anasema, "Hakuna meli inayokosa nanga. Matishio ni mengi na hasa wakati nikiwa katika nafasi ya RCO. 

"Nilipata vitisho vingi nikiwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mara, Mwanza na Dodoma kabla sijapangiwa majukumu ya RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa) Rukwa, Lindi, Shinyanga, Kagera na mwanzilishi Kanda Maalum ya Dar es Salaam. 

"Kujibu swali lako, vitisho vya moja kwa moja nikiwa nafasi za RCO mikoa hiyo vilikuja kwa muundo huu, ‘Hili umelionea, nitahakikisha huwi RCO tena hapa. Nitahakikisha matukio yote ambayo umeyafanya na mahali ulikofanya rushwa tutaweka hadharani. Kesi fulani usiifuatefuate’. 

"Matishio mengine ya ana kwa ana yalikuwa yakifanywa na mahabusu walioko tayari gerezani na wanaoandaliwa kupelekwa gerezani. 

"Yalikuja kwa mtazamo huu, ‘Unajifanya wewe ndiye unajua kufuata taratibu, nitahakikisha nikitoka ama wewe mwenyewe ama anayekuhusu au mali zako nimeshatoa maagizo watu wafuatilie," anasema. 

WIZI SHULENI 

Kamanda Mssika anakumbuka kesi ya wizi ya mamilioni ya shilingi katika Shule ya Sekondari Weruweru, mkoani Kilimanjaro, ambako mhasibu shuleni huko alituhumiwa kughushi saini ya aliyekuwa Mkuu wa Shule hiyo na kuitumia katika vocha za shule. 

"Upelelezi ulianza akiwa ameshatoroka, ilituchukua muda mrefu. Chanzo cha taarifa kutoka Bagamoyo kilitutaarifu alikuwa amekimbilia huko, tukaandaa safari kupitia Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na polisi wa eneo husika, tukaenda kwa siri. 

"Tukiwa Bagamoyo, mbinu ya upelelezi tuliyotumia, kwa sababu nilikuwa mzoefu katika masuala ya uuguzi, tulitumia mavazi ya uuguzi na vifaa vya hospitalini kuanza upelelezi wa tukio hili. 

"Taarifa ikaja yuko kijiji kimoja kwa nyanya wake (bibi). Wakati huo utakumbuka taarifa tulikuwa tunazikusanya tukiwa na kofia kama wauguzi na madaktari. 

"Utekelezaji eneo la tukio tulikwenda kiaskari, tukavamia nyumba ya bibi yake. Bibi huyo aliaminika kipindi hicho kuwa kati ya viongozi wanaojihusisha na uchawi katika eneo lile. 

"Tulipofika eneo la tukio nyumbani kwa bibi huyo, tulipoingia katika sebule yake, tulikuta ndege wamekaushwa na miguu ikining’inia. Alishtuka kutuona. Swali la kwanza ni wapi aliko Omar Madongo? (mtuhumiwa). 

Kutokana na mshtuko, bibi huyo hakuwa na majibu, lakini kijana aliyetuongoza kwenda hapo akanieleza kuwa mtuhumiwa hakuwa katika nyumba hiyo, bali alikuwa amejificha katika nyumba nyingine na walipoivamia hakukuwa na dalili za mtu kuishi humo. 

"Ng’ambo ya barabara kulikuwa na gari ambalo mtuhumiwa alitoroka nalo Moshi. Kulikuwa na vibanda vitatu, kimoja kimezibwa sehemu zote na sehemu ya juu iko wazi, liliwekwa lile gari. 

"Alinunua nyumba akaitengeneza vizuri ili gari lienee humo, hata mpitanjia asiweze kuona. Tulibomoa nyumba, gari likiwa ndani na lilikuwa na mafuta yaliyojaa na lita zingine 20 kwenye dumu. Mtuhumiwa alikuwa maarufu mjini Moshi na Arusha kwa sababu alikuwa na fedha. 

"Tukiwa mjini Bagamoyo, tulipokea simu kutoka kwa ndugu yake akituarifu, 'mtuhumiwa yupo  Kituo cha Polisi Magomeni, Dar es Salaam' na tulipokwenda tulimkuta na ndipo tulipomchukua kwenda naye Moshi (ilikokuwa kesi yake)," anasimulia. 

Kamanda Mssika anasema kuwa kutokana na umaarufu wa mtuhumiwa huyo, alipokea vitisho kutoka kwa watu (bila kuwataja), walimtishia na hata kujaribu kumkatisha tamaa kwamba atahamishwa eneo la kazi. 

"Vilikuja kwa njia mbalimbali. Mpaka vitisho vya uganga. Wakati tunakwenda mahakamani, watu walikuwa wanatupa vitu kwenye njia niliyokuwa ninapita kwa lengo la kunitishia na kunikatisha tamaa, lakini hatimaye alihukumiwa kifungo chini ya Jaji Kileo," anasimulia. 

JESHI KULALAMIKIWA 

Kamanda Mssika anasema anaweza asiwe na majibu ya moja kwa moja kwanini watu hulalamikia Jeshi la Polisi kutokana na utendaji wa askari wake. 

"Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kulinda raia na mali zao. Kunapotokea malalamiko ya aina yoyote, kwanza ni pongezi kwa wananchi kwa jumla, lakini ni pongezi kwa wanaolalamika. 

"Majibu ya moja kwa moja kwamba ni sababu ipi inayopelekea, ushauri wangu kila malalamiko yajadiliwe kulingana na tukio husika. 

"Malalamiko yanapojitokeza, hasa upande mmoja ni lazima yawe na majibu ya pande zote mbili, wananchi wanalalamika, hii ni kwa ujumla. Kama wanalalamika mfano kesi haziendi sawa au kukamatwa isivyo, mimi binafsi ninaona malalamiko ya jumla yakizingatiwa kuna uwezekano kupata matokeo ya sababu ya kijumla. 

"Nikizungumzia uzoefu, malalamiko mengi yanayotolewa yanafikishwa polisi, wanayapokea na kufanya uchunguzi mpaka kufika hatua ya mwisho. 

"Tumelalamika namna hii, polisi imelishughulikia na kuchunguza na kubaini moja, mbili, tatu. Hiyo ikifanyika, inaweza kuondoa mawingu mbalimbali kwamba mrejesho unafanyika," anasema. 

Kamanda Mssika anasema kwa uzoefu wake katika kazi hiyo, malalamiko yanayowasilishwa kwa Jeshi la Polisi ni yale ambayo tukio limetokea leo, mtu amebaki nalo hakulitolea ripoti kwa wakati mwafaka. 

Anasisitiza kwamba polisi kuna kitengo maalumu cha uchunguzi wa malalamiko ya polisi yanayofikishwa huko. 

Kamanda Mssika anasema maboresho yanayofanywa Jeshi la Polisi katika uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni makubwa. 

"Tumeshuhudia kuundwa Tume ya Haki Jinai, ninaamini imempelekea Rais ya ziada ambayo yameanza kufanyiwa kazi. 

"Jeshi la Polisi katika usasa ndiko lilikojikita. Linashirikiana kimataifa, hivyo huwezi kubaki nyuma wakati majeshi mengine ya kimataifa yanakwenda mbele kwa teknolojia," anasema. 

Kamanda Mssika anasisitiza hatua hiyo iendelee na kushauri Programu ya Polisi Jamii nayo iboreshwe zaidi. 

WALIOKALIA KITI 

Kamanda Mssika anasema, "Kwa watendaji Jeshi la Polisi, jamii uliyonayo ukiwa kwenye kiti ndiyo hiyohiyo itakupokea ukiondoka katika kiti. 

"Hivyo, polisi jamii inabidi ianze nyumbani, ndani ya Jeshi la Polisi, uhusiano, utekelezaji wa kweli na ushirikiano na wananchi uwe endelevu. 

"Uelewa wa wananchi ni mkubwa, wanapima kwenye mizani utendaji wa polisi na malalamiko hayaji Jeshi la Polisi kwa jumla, yanalenga kwa baadhi ya matukio ambayo hayaripotiwi na kurekebishwa," anasema. 

Kamanda Mssika anashauri wasiitwe kufafanua malalamiko yao kama tuhuma, bali zitumike kama fursa kuzifanyia kazi na kuzitafsiri kwanini zimejitokeza na kuziondoa. 

"Unapofikiri haliwezi kuhesabika, linahesabika hatua kwa hatua na huwezi kujua kama linahesabika mpaka hapo umeondoka ndani ya jeshi, upo uraiani," anasema. 

Kamanda Mssika pia anashauri watendaji ndani ya jeshi hilo kuzingatia utendaji wa haki wanapokuwa katika meza zao na si kuchanganya na tamaa ya aina yoyote, yao binafsi au kufanya kwa niaba. 

"Mbegu unayoipanda leo, inakuja kujibu ukishaondoka. Uhusiano unaojenga leo uwe wa kutenda haki kwa maana kama mhalifu, haki yake apatiwe kwa yale aliyofanya. 

"Ukitenda haki kila mtu anajua 'hii ilikuwa haki yangu, kama ni kufungwa mimi ni mhalifu'. Ukitenda haki ni njia moja wapo ya kuimarisha uhusiano kupitia programu ya polisi jamii," anasema. 

Kamanda Mssika hadi kustaafu kwake, ana nishani ya vita ya mstari wa mbele, nishani ya utumishi mrefu na tabia njema na nishani ya utumishi uliotukuka ndani ya Jeshi la Polisi. 

Hivi sasa anaandaa kitabu ambacho pamoja na mambo mengine, kinahusu maisha yake kwa ujumla katika ajira, kuanzia kazi aliyofanya hospitalini Muhimbili, Jeshi la Polisi na anachofanya kwa sasa.