Wananchi watumie muda uliowekwa kujiandikisha uchaguzi wa S/Mitaa

Nipashe
Published at 10:46 AM Oct 16 2024
Rais Samia Suluhu Hassan
Picha:Mtandao
Rais Samia Suluhu Hassan

KAZI ya kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa inaendelea sehemu mbalimbali nchini. Wakati hilo likiendelea, viongozi wakuu kitaifa wamekuwa wakiwahimiza wananchi kushiriki mchakato huo ili kuwa na sifa za kuwachagua viongozi wanaofaa.

Viongozi hao si tu wanafanya hivyo kinadharia bali kwa vitendo kwa sababu wameshuhudiwa wakijiandikisha katika maeneo yao ili nao washiriki kuwachagua watu watakaosimamia shughuli za maendeleo na kuwaongoza wananchi kutatua changamoto zilizoko kwenye sehemu husika. 

Katika kufanya hivyo, wakati wa kufunguliwa kwa pazia la kujiandikisha, Rais Samia Suluhu Hassan alifanya hivyo Chamwino mkoani Dodoma huku Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango akijiandikisha nyumbani kwao, Buhigwe mkoani Kigoma. Mbali na Rais na makamu wake, viongozi wengine kama vile mawaziri na wakuu wa mikoa wamejiandikisha huku wakiwataka wananchi waige mfano huo. 

Viongozi hao wametoa kauli mbalimbali kuelezea umuhimu wa kushiriki uchanguzi huo na kuonya kuwa asiwapo mtu yeyote wa kufanya hujuma katika mchakato mzima. Rais Samia, kwa mfano, ameonya mara kadhaa kuhusu dosari zozote zitakazojitokeza huku akitaka uchaguzi huo usilitie doa taifa.   

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliopangwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu, ni wa muhimu na wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi bora watakaosukuma gurudumu la maendeleo katika maeneo husika. Viongozi na wananchi hao ndio wanaojua kwa undani matatizo yanayowakabili, hivyo kuchagua viongozi bora ni hatua mojawapo ya kuyatatua. 

Kwa mantiki hiyo, jambo la muhimu ni wananchi kujiandikisha na kufanya mchakato katika kura za kuchagua wagombea wenye sifa katika ngazi ya chama. Uchaguzi huu ndilo chimbuko rasmi la demokrasia na utawala bora, kwa hiyo ni muhimu kila mwananchi mwenye sifa za kushiriki asikose. 

Kupitia serikali za mitaa, wananchi kwa kushirikiana na viongozi wao, wana uwezo wa kuainisha kero zinazowakabili na kutafuta mbinu za kuzishughulikia pamoja na kujiletea maendeleo endelevu. 

Kero kama vile maji, barabara, kilimo, mifugo, afya na elimu katika maeneo husika, watatuzi wa kwanza ni wananchi wenyewe. Kupita  uchaguzi wa serikali za mitaa, kwa kuchagua viongozi bora ndilo suluhisho katika kutatua kero hizo.  

Kama wahenga wasemavyo kwamba majuto ni mjukuu, wananchi wajitokeze kujiandikisha kwa ajili ya kushiriki uchaguzi huo muhimu kwa mustakabali wao na kinyume cha hapo watajikuta hawapigi hatua kutoka walipo sasa kwa sabau ya kutokushiriki. Kawaida, baadhi ya wananchi wamekuwa wazito katika kushiriki uchaguzi na matokeo yake wanapopatikana viongozi wabovu au wasiofaa, hujikuta wakilaumu bila kujua kosa limeanzia kwao. 

Kama alivyosema Rais Samia juzi kwamba uchaguzi wa serikali za mitaa ni muhimu kwa sababu utasaidia unaonesha ushiriki wao katika masuala ya maendeleo sambamba kubuni, kupanga na kutekeleza mipango yao, Watanzania kamwe wasikose kushiriki kwenye mchakato huo kwa manufaa yao. 

Ni vyema wananchi wakatumia muda uliopangwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wakazi ili kuwa na sifa za kupiga kura. Viongozi katika mitaa na vyama vya siasa ni muhimu wakaendelea kuwahimiza wananchi kujiandikisha ili kupata nafasi ya kupiga kura siku ya uchaguzi itakapowadia.