Kasi iongezwe mapambano dhidi ya tatizo la udumavu

Nipashe
Published at 10:51 AM Oct 10 2024
Udumavu.
Picha:Mtandao
Udumavu.

TATIZO la udumavu kwa watoto nchini limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu huku serikali ikichukua hatua katika kukabiliana nalo kwa kushirikiana na wadau wa ndani na wa nje. Kwa namna linavyozungumzwa linaonesha kuwa bado ni kubwa na lina athari kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mtoto anapodumaa maendeleo yake ya ukuaji yanakuwa ya shida na hata uwezo wake wa kufanya mambo kwa ufanisi, kuanzia darasani hadi kwenye maisha yake ya kila siku, unakuwa mdogo. Kwa mantiki hiyo, mtu kama atakuwa na udumavu tangu akiwa mdogo, utendaji kazi wake utakuwa mdogo, hatakuwa na tija na atashindwa kufanya mambo mengi kwa sababu ya uwezo mdogo wa kufikiri.

Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2022 kuhusu udumavu, theluthi moja ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wamedumaa. Takwimu hizo zinaonesha kwamba kati ya watoto watatu, mmoja ana udumavu hali inayoashiria kuwapo kwa hatari ya kuporomoka kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa ufungwaji wa mkutano wa wadau wa lishe nchini uliofanyika Mwanza hivi karibuni, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Jesca Lebba, alisema kwa sasa, hali ya udumavu katika Mkoa wa Mwanza ni asilimia 28, ikiwa imepungua kutoka asilimia 39 mwaka 2018. Hali hii inaashiria mwelekeo mzuri, huku lengo la taifa likiwa ni asilimia 30.

Dk. Lebba, alisema katika mkoa huo, halmashauri zinazokabiliwa zaidi na tatizo hilo ni Ukerewe, Buchosa na Kwimba, lakini jitihada zinafanyika kuboresha hali hiyo. Alisisitiza kuwa mikakati mbalimbali inafanyika ili kupunguza tatizo hilo kwa kuwa wanaamini kwamba lishe ni muhimu kwa maendeleo ya binadamu na bila kuwa na afya njema, mtu hawezi kufanya chochote.

Mtaalamu huyo wa afya alisema tatizo kubwa linalochangia kuwapo kwa hali hiyo ni kukosa lishe bora ambayo inahitaji vyakula kutoka makundi sita. Hali hiyo, alisema haizingatiwi na wakazi wa mikoa huo ambao wengi ni wavuvi na kutokutumia samaki wanaovua badala yake huuza. Pia kwa mujibu wa Dk. Lebba, watu wengi hawatumii mboga za majani na matunda.

 Licha ya kuwapo kwa takwimu hizo, inaelezwa kuwa kumekuwa na mafanikio makubwa katika kupunguza tatizo hilo kwa mikoa mitano ya Tanzania Bara kutoka mwaka 2016 hadi 2022 kwa wastani wa asilimia 10. Mikoa hiyo na asilimia kwenye mabano ni Mtwara (15.7), Tanga (14.9), Lindi (13.7), Mwanza (11.1) na Kigoma (10.9).

Pamoja na kuwapo kwa matumaini hayo ya kupungua kwa udumavu, inasikitisha kuona kwamba mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwamo Iringa, Njombe, Mbeya na Rukwa ambayo ni wazalishaji wakubwa wa vyakula ndiyo inaongoza kuwa na tatizo hilo. Sababu kubwa ya kuwapo kwa hali hiyo, kwa mujibu wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Tawala za Mikoa ni jamii ya watu wa mikoa hiyo kutozingatia ulaji sahihi wa vyakula.

Ni wazi kwamba serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na tatizo la utapiamlo na udumavu ambavyo vina uhusiano mkubwa ikiwamo kutoa elimu ya lishe kwa wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na shuleni. Pia serikali imeweka suala la lishe kama kipaumbele muhimu katika kutekeleza mipango ya maendeleo ya taifa.

Juhudi hizo za serikali zinapaswa kupongezwa na kuungwa mkono na wadau mbalimbali zikiwano asasi za kiraia ambazo nimejipambanua katika kupambana na afya ya watu ili kuwa na jamii yenye siha kwa maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.

Hakuna maendeleo ya taifa lolote yanayoweza kupatikana kama jamii ina tatizo la afya ikiwamo utapiamlo na udumavu, hivyo ili nchi isonge mbele kijamii na kiuchumi katika sekta kama kilimo, viwanda, biashara, ufugaji na uvuvi, jambo la msingi la kuzingatiwa ni kupambana na utapiamlo na udumavu.