Hongera Yanga Princess kwa usajili, Simba Queens jiulizeni

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:14 AM Oct 05 2024
Hongera Yanga Princess kwa  usajili, Simba Queens jiulizeni
Picha:Mtandao
Hongera Yanga Princess kwa usajili, Simba Queens jiulizeni

JUMATANO iliyopita niliitazama mechi ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii ya Wanawake kati ya Simba Queens dhidi ya Yanga Princess, nikagundua baadhi ya vitu ambavyo si wengi ambavyo walivitarajia.

Kwanza kabisa wengi walidhani Simba Queens ingeshinda mechi hiyo kirahisi kama ambavyo huwa inafanya, lakini haikuwa hivyo.

Kila mmoja alijua Yanga Princess ingeteseka katika mchezo huo kutokana na wapinzani wao kuwa na kikosi bora na imara, lakini ilikuwa kinyume chake.

Mechi iliisha kwa Yanga Princess kushinda penalti 4-3, baada ya sare ya bao 1-1 dakika 90 za kawaida.

Almanusura mechi imalizike kwa bao 1-0, kama si goli la dakika za majeruhi la Mkenya, Jentrix Shikangwa.

Kwa jinsi mchezo ulivyochezwa kwa dakika zote 90, isingekuwa haki kama Yanga Princess ingepoteza, hata kwenye mikwaju ya penalti.

Ilistahili kushinda, na kweli ikashinda hata timu hizo zilipokwenda kupigiana mikwaju ya penalti.

Hata kwenye matuta pia, Yanga Princess ilistahili kushinda kwa jinsi wachezaji wake walivyokuwa makini kwenye upigaji pamoja na umahiri wa kipa wao mpya, Rita Akarekor, anayeichezea timu ya taifa ya Nigeria, akisajiliwa kutoka Delta Queens ya nchini humo.

Inaonekana ni kama viongozi wa Simba Queens hawakujiandaa vyema timu yao kuelekea kwenye mchezo huo.

Hata tukio la ucheleweshwaji wa vibali vya wachezaji wa kigeni ambao ni tegemeo, akiwamo Vivian Corazone,  Elizabeth Wambui, Shikangwa, Precious Christopher na wengineo unaonyesha hivyo.

Waliingia dakika chache kabla ya mapumziko baada ya kukamilisha taratibu, lakini tayari timu ilikuwa imeshapachikwa bao. Kuingia kwao kidogo timu ilitulia.

Pamoja na matatizo hayo, ukiangalia kiwango cha Simba Queens kimepungua na si kama ilivyokuwa misimu miwili iliyopita.

Kuna wachezaji wachache sana ambao wanaweza kuibeba timu hiyo, lakini wengi kwa sasa wanaonekana wameshuka viwango.

Hata upande wa golikipa pia unaonekana kuna matatizo na linatakiwa kufanyiwa kazi haraka sana kwa kusajili kipa imara mwenye hadhi ya michuano ya kimataifa.

Pia inaonekana wachezaji ni wazito kama vile hawafanyi mazoezi ya stamina na pumzi, tofauti na wenzao wa Yanga Princess.

Nadhani tayari viongozi na wachezaji walishaanza kubweteka baada ya kuona hawapati upinzani mkubwa zaidi wanapokutana na timu moja tu ya JKT Queens.

Kiwango cha timu hiyo kilianza kutia shaka kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Kanda ya CECAFA iliyofanyika hivi karibuni huko Ethiopia, ambapo haikufanya vyema, ikipoteza michezo yake dhidi ya timu ambazo kama ingekuwa bora kama ambavyo huwa, isingefungwa. 

Kinachotakiwa sasa kipindi cha dirisha dogo ifikapo Desemba, kwa kuondoa baadhi ya wachezaji wasio na tija, na kusajili wengine wanaoongeza nguvu na chachu kikosini kwa sababu wengi wanaonekana wamesharidhika.

Pongezi ziende kwa viongozi wa Yanga Princess ambao hawakuwa na makeke, wakasajili wachezaji wengi wazuri, ambao miguu yao ndiyo iliyoongea uwanjani.

Wachezaji kama Angela Chineneri, JKT Queens, Arieth Udong, Agnes Palangyo, Rita, Uzoamaka Igwe na wengineo wameongeza nguvu na ubora mkubwa katika kikosi hicho ambacho kinaonekana kitaleta upinzani mkubwa katika harakati za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania msimu huu.

Vyovyote itakavyokuwa katika mchezo wa fainali leo hii dhidi ya JKT Queens, lakini msimu huu Yanga Princess imetengeneza kikosi bora ambapo kinaonekana ni tishio.