Ufunguzi msimu mpya Ligi Kuu ya Wanawake wavutia

Nipashe
Published at 07:12 AM Oct 05 2024
Ufunguzi msimu mpya Ligi  Kuu ya Wanawake wavutia
Picha: Mtandao
Ufunguzi msimu mpya Ligi Kuu ya Wanawake wavutia

FAINALI ya Ngao ya Jamii kwa Wanawake kwa mwaka huu inatarajiwa kufanyika leo kwa kuwakutanisha 'Maafande' wa JKT Queens dhidi ya Yanga Princess, zote kutoka jijini Dar es Salaam.

JKT Queens ilifika hatua hiyo baada ya kuibamiza bila huruma Ceasiaa Queens kutoka Iringa mabao 7-0 wakati Yanga Princess ilipata ushindi wake wa kwanza wa penalti 4-3 dhidi ya watani zao, Simba Queens kutokana na kwenda sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 90 za kawaida.

Mashindano hayo yanafanyika kwa mwaka wa pili baada ya mwaka jana yalipoanza, Simba Queens kufanikiwa kuibuka mabingwa.

Kuanza kwa mashindano hayo ni ishara ya ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania umekaribia, ligi hiyo inayotarajiwa kushirikisha timu 10 kutoka mikoa mbalimbali itaanza rasmi ifikapo Oktoba 9, mwaka huu.

Timu zinazotarajiwa kushiriki ligi hiyo ya juu ya wanawake nchini ni pamoja na mabingwa watetezi, Simba Queens, JKT Queens, Yanga Princess, Ceasia Queens, Fountain Gate Princess, Alliance Girls, Mashujaa Queens (zamani Amani Queens) na Bunda Queens ya Musoma mkoani Mara.

Gets Program ya Dodoma na mabingwa wa kwanza wa Ligi Kuu ya Wanawake kwa msimu wa 2016/2017, Mlandizi Queens kutoka Mlandizi mkoani Pwani pia zitashiriki ligi hiyo baada ya kupanda daraja.

Kufanyika kwa mashindano hayo ni kielelezo cha wazi kwamba mpira wa miguu wa wanawake Tanzania unaendelea kupiga hatua, michuano hiyo imeonekana kuvutia na timu zilizocheza mechi za hatua ya nusu fainali kila moja ilionyesha kiwango kizuri, bila kujali matokeo ya mwisho.

Wachezaji wa timu zote nne, walicheza katika kiwango cha juu na chenye ushindani kutokana na kila timu kufanya  maandalizi mazuri kwa sababu ya kuhitaji kutinga fainali na hatimaye kubeba taji hilo.

Licha ya kuwapo kwa dosari chache kabla ya kuanza kwa mechi hizo, Ceasiaa wakichelewa kufika uwanjani kama kanuni za mchezo zinavyoelekeza huku benchi la ufundi la Simba Queens likilazimika kupangua kikosi kutokana na wachezaji wake baadhi wa kikosi cha kwanza ambao ni raia wa kigeni kutokuwa na vibali.

Kuchelewa kupatikana kwa vibali kwa wachezaji hao wa Wekundu wa Msimbazi kulizua sintofahamu, lakini taratibu na kanuni za nchi ziliheshimiwa mpaka pale walipopata vibali ndio wakaruhusiwa kuingia mchezo isipokuwa kocha mkuu wa timu hiyo na nyota wengine watatu, ambao nyaraka zao hazikukamilika.

Ukiondoa taratibu hizo za kiutawala, mashabiki waliofika kwenye Uwanja wa KMC Complex walipata burudani na hii inaonyesha katika msimu mpya mambo yatazidi kuwa bora kwa sababu hakuna timu ndogo au timu inayoingia uwanjani na matokeo 'mfukoni'.

Hongera kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake Tanzania (TFF), na Kamati ya Soka la Wanawake kwa kuhakikisha kandanda kwa wanawake linaendelea kusonga mbele kadri siku zinavyokwenda.

Ni ukweli usiofichika kuwa na Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania yenye ushindani, Ligi ya Wanawake Daraja la Kwanza imara na Ligi ya Mabingwa wa Mikoa yenye ubora, ndio 'kisima' sahihi kinachozalisha wachezaji wanaoitwa kwenye timu za taifa.

Ili kuhakikisha malengo ya TFF na TWFA yanafikiwa, huu ni wakati wa mikoa kuanza pia maandalizi ya timu zao zilizoko katika Ligi Daraja la Kwanza lakini pia kuzitaka klabu zinazotarajiwa kushiriki Ligi ya Mabingwa wa Mikoa kujiweka tayari kwa ushindani huku wakihakikisha wanaendesha ligi na si kusimamia mashindano ya muda mfupi.

Mikoa inayowakilishwa na mabingwa waliotokana na michuano ya 'zimamoto' matokeo yake huonekana mapema kwa wachezaji kushindwa kwenda na kasi na kusababisha kupokea vichapo vya aibu au kuwa wasindikizaji na kushindwa kupeperusha vyema bendera za mikoa wanayotoka.

Licha ya uwekezaji katika soka la wanawake kuwa ni changamoto, hili lisiwape 'mwanya' viongozi wa mikoa kuacha kuandaa vyema timu zao na kwa kufanya hivyo itawapelekea kila mwaka washindwe kupanda daraja.