Butondo kutoa mifuko 100 ya saruji ujenzi Zahanati Mwasele

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 05:32 PM Oct 09 2024
Mwananchi wa kijiji cha Mwasele wilayani Kishapu Said Hamis akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo.
Picha:Marco Maduhu
Mwananchi wa kijiji cha Mwasele wilayani Kishapu Said Hamis akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo.

MBUNGE wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo,ameahidi kutoa mifuko 100 ya saruji ili kufanikisha ujenzi wa Zahanati katika kijiji cha Mwasele wilayani Kishapu.

Ametoa ahadi hiyo jana kwenye mkutano wa hadhara wakati akizungumza na wananchi wa Mji wa Mhunze wilayani Kishapu, pamoja na kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi. 

Alisema kutokana na kijiji cha Mwasele kutokuwa na Zahanati, hivyo amemuagiza Diwani wa Kishapu Joel Ndetoson, kukaa na viongozi wa kijiji ili watafute eneo ambapo itajengwa Zahanati hiyo, na kwamba atawaunga mkono kwa kutoa mifuko 100 ya saruji. 

“Huduma za afya ni muhimu sana kuwa karibu na wananchi, nitatoa mifuko 100 ya saruji ili ujenzi wa Zahanati uanze mara moja, ombi lenu kwenu pamoja na diwani tafuteni eneo la kujengwa Zahanati hiyo, na likifika hatua ya renta nitambana Mkurugenzi aimalizie kujenga,”alisema Butondo. 

Nao baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mwasele akiwamo Said Hamis, wakiwasilisha kero kwa mbunge huyo, wamesema tatizo lao kubwa ni kwamba hawana Zahanati kijijini humo, na hivyo kupata shida ya kufuata matibabu umbari mrefu, na kumuomba mbunge awasaidia kutatua tatizo hilo.