Nchimbi aagiza m’biashara kulipwa madai ya miaka 12

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 11:18 AM Oct 09 2024
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi, Dk. Emmanuel Nchimbi
Picha: CCM
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi, Dk. Emmanuel Nchimbi

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi, Dk. Emmanuel Nchimbi, ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Meatu, mkoani Simiyu kumlipa mfanyabiashara ndani ya mwezi huu madai yake ya Sh. milioni 38 alizosotea kwa miaka 12.

Mfanyabiashara huyo alimlalamikia Dk. Nchimbi akiwa katika mkutano wa hadhara wilayani Meatu, mkoani Simiyu, akidai fedha hizo tangu mwaka 2012, lakini mpaka sasa hajalipwa licha ya kuwa na nyaraka zote.

Baada ya Dk. Nchimbi kusikiliza lalamiko lake aliagiza halmashauri hiyo imlipe haraka iwezekanavyo.

"Huyu aliyelalamika mbele yangu mwezi huu usiishe, alipwe fedha zake na ninakupa namba yangu ili usipolipwa uniambie," alisema Nchimbi huku akishangiliwa na wana-Meatu.

Awali, Dk. Nchimbi alizitaka taasisi za serikali na halmashauri nchini kutotangaza zabuni ikiwa hawana bajeti ili kuiepusha serikali na mzigo wa madeni.

Pia, alikemea baadhi ya viongozi serikalini kutanguliza mbele maslahi yao binafsi na kwamba wapo baadhi ya viongozi ambao wakipata nafasi wanaanza kutanguliza mbele familia zao.

Kutokana na hali hiyo, alisema CCM itaendelea kushirikiana na serikali kupambana na wanaohujumu miradi na kazi nzuri zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, alisema timu yake ya kuangalia kero imeongea na wananchi 48 ambao wamewasilisha kero 89 ambazo zimekabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa (Kenani Kihongosi) na ofisi yake imechukua namba za simu kwa ajili ya kuwasiliana nao kuona kama wamesaidiwa. 

Kuhusu kero iliyowasilishwa na mmoja wa wakazi kuhusu Shule ya Msingi Mwangudo kutokamilika kwa wakati, Nchimbi alimwita Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Faudhia Ngatumbara ambaye alifafanua kwa kusema:

“Jitihada za ujenzi zinaendelea na matarajio yao mpaka kufikia Januari mwakani itakuwa tayari imeanza kupokea wanafunzi,” alisema. 

Nchimbi aliahidi ofisi yake itachangia Sh. 10,000,000 kuhakikisha shule hiyo inakamilika kwa wakati.

Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amosi Makalla, alisema hawatasimamisha wagombea wenye makandokando katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 27, mwaka huu.

“Niwahakikishie CCM itawaletea wagombea safi wanaokubalika kufanyakazi na wananchi, hivyo muwapigie kura wagombea wa CCM.

“Hatutadiriki hata kidogo kuwaletea watu ambao wanamkandokando na sisi hatuna haja ya kusimamisha wagombea ambao tutahangaika kuwasafisha kwa dodoki, hivyo tutawaletea watu safi.”

Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Abdallah Hamid, alisema zawadi ya serikali kwa wananchi wa Meatu ni kujenga vituo viwili vya zana za kilimo ambayo kila kimoja kitakuwa na trekta 20.

Alisema kupitia vituo hivyo mwananchi atalima kwa kutumia trekta hizo kwa gharama ya Sh. 40,000 kwa ekari ingawa serikali ina mpango wa kushusha zaidi kiwango hicho.

CHADEMA

Katika mkutano uliofanyika eneo la Luguru wilayani Itilima Mwenyekiti wa CHADEMA Wilaya ya Meatu, Terry Kilugala, Katibu wake Gershon Mipawa pamoja na wanachama wao zaidi ya 60 walihamia CCM na kupokewa na Nchimbi.  

Akizungumza baada ya kupokewa Kilugala, alisema wameshawishika kutokana na utendaji kazi wa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Tulikuwa tunaenda Mwanza siku mbili kwa ubovu wa barabara, leo tunaenda na kurudi. Lazima tuseme ukweli, CCM imefanya kazi.

Balozi Nchimbi, akiwapokea, alisema: “Hawa ndugu zetu wameona mbali mapema, maana viongozi wakubwa kama Peter Msigwa kaona shida zao, wewe unasubiri nini? Rudini CCM, na nawapongeza wote mliojiunga na CCM, viongozi pamoja na wanachama. Karibuni sana tufanye kazi ya kujenga taifa pamoja.”

Kadhalika, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kushiriki uchaguzi ili waweze kupata nafasi ya kuchagua viongozi wa chama hicho akitamba ndio wana uwezo na maarifa ya kuongoza nchi.