Mulokozi awapa mbinu za kiuchumi wahitimu wa kidato cha 4 Shule ya Ujenzi

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 08:04 PM Oct 08 2024
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ujenzi.
Picha:Yasmine Protace
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ujenzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa MATI BRANDS LTD, David Mulokozi, amewapa wahitimu wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Ujenzi mbinu muhimu za kufanikiwa kiuchumi katika maisha yao ya baada ya kumaliza shule.

Mulokozi, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya shule hiyo iliyopo Mkuranga, Mkoa wa Pwani, alisisitiza umuhimu wa kumtanguliza Mungu, kuwa na nidhamu, na kuheshimu muda kama misingi muhimu ya mafanikio.

Akizungumza na wahitimu hao, Mulokozi alisema, "Imani kwa Mungu na nidhamu ni siri za mafanikio katika biashara. Heshimu muda na zingatia kazi unayofanya kwa bidii." alisema kuwa vijana wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii, akibainisha kuwa kampuni yake imeajiri vijana wengi ambao wamechangia kukuza biashara zake.

Katika hotuba yake, Mulokozi pia aliahidi kuwasaidia wahitimu wa shule hiyo kwa kutoa msaada wa vifaa vya kufundishia.

Aliwaahidi kuwapatia runinga tatu na kushirikiana na uongozi wa shule katika kujenga uwanja wa michezo, changamoto ambazo shule hiyo imekuwa ikikabiliana nazo kwa muda mrefu.

Mkurugenzi Mtendaji wa MATI BRANDS LTD, David Mulokozi.

Mbali na hayo, mmoja wa wasaidizi wa Mulokozi aliahidi kuchangia shilingi milioni 3.2 kwa ajili ya kununua vitabu vya ziada na kiada, huku Mulokozi akiahidi kutoa shilingi milioni 5 kwa ajili ya walimu wa shule hiyo kama motisha kwa kazi yao ngumu ya kufundisha.

Pia, alitoa shilingi 800,000 kwa ajili ya wanafunzi wa kikundi cha "The Giant" kutoka Shule ya Sekondari St. Matthew's iliyopo Mkuranga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya MHL Advocate, Peter Mutembei, alimpongeza Mulokozi kwa kushiriki katika hafla hiyo kama mgeni rasmi, akimwelezea kama mfanyabiashara mkubwa mwenye ushawishi ndani na nje ya Tanzania.

"Wengi wamekusikia tu, lakini leo wana nafasi ya kukutana nawe na kupokea baraka zako," alisema Mutembei kwa furaha.

Shule ya Ujenzi inajivunia mafanikio makubwa katika ufaulu wa wanafunzi wake, huku ikisisitiza malezi, usalama, na elimu bora kama misingi ya maendeleo ya wanafunzi wake.

1